Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu watatu wapoteza maisha ajali ya malori Bukombe

Kifo Mautii Watu watatu wapoteza maisha ajali ya malori Bukombe

Thu, 11 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu watatu wamepoteza maisha na wengine wanane kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha malori matatu yaliyogongana eneo la Butibili, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo wakati akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu akisema imetokea usiku wa kuamkia leo Januari 11, 2024 saa nne usiku baada ya lori lililokuwa limebeba mchele kuharibika na dereva kuacha kutoa tahadhari kwa madereva wenzake.

Amesema waliopoteza maisha ni dereva na utingo wa lori pamoja na utingo wa basi huku majeruhi wanane wakiwa ni dereva wa basi la Abood aliyevunjika mkono na abiria wa gari hilo waliopata majeraha madogo madogo ambao wanaendelea na matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo.

Akielezea tukio hilo, Nkumba amesema lori lililokuwa limebeba mchele likitokea Ushirombo liliharibika eneo la Butibilina lakini dereva hakutoa tahadhari kwa madereva wenzake.

Amesema lori lingine lilifika na kumgonga kwa nyuma na baadaye lori lingine likitokea Runzewe likamgonga kwa mbele na kusababisha vifo hivyo.

“Baadaye wakati ajali hiyo imeshatokea ilikuwa saa nane usiku basi la Abood likitokea Ushirombo, dereva bila kuchukua tahadhari ghafla alikutana na ajali mbele yake na alijitahidi kuokoa abiria akakata kona kuingia pembeni ndio akawa amevunjika mkono na abiria wake saba wamepata majeraha kidogo wanaendelea na matibabu,” amesema Nkumba aliyetembelea eneo la tukio usiku.

Amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori lililokuwa limebeba mchele kutochukua tahadhari ya kuweka alama ili kutoa ishara kwa madereva wenzake wanaotumia barabara hiyo kuu.

Nkumba amewataka madereva kuchukua tahadhari pindi wanapopata hitilafu barabarani na kukemea mwendo kasi unaofanywa na madereva wa malori hususan nyakati za usiku.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo akieleza kuwa waliopoteza maisha ni dereva na utingo wa lori na wa basi.

Juhudi za kumpata mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe kujua hali za majeruhi zinaendelea kufanyika

Chanzo: www.tanzaniaweb.live