Watu watano wamefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye madimbwi na visima vya maji mkoani Simiyu.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Mei 23, 2022 kaimu kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Faustine Mtitu amesema kuwa vifo hivyo vimetokea ndani ya wiki moja katika matukio matatu tofauti.
Amesema ndani ya wiki moja Jeshi hilo limepokea taarifa za matukio matatu ya watu kutumbukia kwenye madimbwi na visima vilivyojaa maji, ambayo yamesababisha vifo vya watu watano.
Mtitu amesema watu watatu kati yao walitumbukia kwa kuteleza wakati wakijaribu kuchota maji kwa matumizi mbalimbali huku wawili wakifariki baada ya kuingia majini kuwaokoa wenzao.
Amesema matukio mawili yalitokea wilaya ya Bariadi na moja lilitokea wilaya ya Maswa.
"Sababu za kutokea kwa matukio haya mfululizo ni pamoja na Kukosekana kwa huduma ya uhakika wa maji hali inasababisha uchimbaji holela wa visima na mashimo katika makazi jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa watoto lakini pia kukosekana kwa umakini wa watumiaji wa mashimo na visima ambavyo vimechimbwa kwenye maeneo yao," amesema.
Advertisement Mtitu amewataka wananchi kuchukua tahadhari za usalama wanapotaka kuchota maji kwenye madimbwi, visima na mabwawa yaliyopo kwenye maeneo yao.
Aidha amewataka wananchi watoe taarifa za matukio kwa wakati kwa kupiga namba ya dharula 114.