Watu sita wamefariki papo hapo na wengine 16 wakijeruhiwa baada ya kugongwa na gari aina ya Hilux double cabin yenye namba za usajili T476 DZL katika eneo la Shule ya Msingi Lumala Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Kaimu Makanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo asubuhi ya leo Julai 22, 2023 wakati kikundi cha vijana kilichotambulika kwa jina la Adden hotel kikiwa kinafanya mazoezi ya kukimbia katika barabara ya sabasaba kuelekea Kiseke wilayani humo.
Msuya amesema msako wa dereva wa gari hiyo unaendelea baada ya kulitelekeza kwenye kituo cha mafuta kisha yeye kutokomea kusikojulika.
Amesema majeruhi 12 wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure huku wanne wakipatiwa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa uangalizi maalum.
“Vijana hao walikuwa wanafanya mazoezi ya mwendo wa pole wakiwa na kundi lao Linalotambulika kwa jina la Adden hotel,”imesema taarifa ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala
Taarifa hiyo kwa umma imesema miili ya marehemu ipo katika Hospitali ya Mkoa Sekou Toure huku taratibu za kuikabidhi kwa ndugu zinaendelea kuratibiwa na hospital ya Sekou Toure na Jeshi la polisi Mkoa wa Mwanza.
“Nitoe pole kwa familia waliopoteza wapendwa wao na tuendelee kuwaweka kwenye maombi majeruhi wote wapate uponyaji wa haraka na waruhusiwe warudi nyumbani kuendelea na majukukumu yao,”amesema Dc Masala