Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu 5,000 hufariki kila mwaka ndani ya Ziwa Victoria

Mvua Ziwa Victoriaaaaaaaa.png Watu 5,000 hufariki kila mwaka ndani ya Ziwa Victoria

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Takriban watu 5,000 wanapoteza maisha kila mwaka kwa ajali za majini zinazotokea ndani ya Ziwa Victoria katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Ziwa Victoria inamilikiwa kwa pamoja na Tanzania (asilimia 51), Kenya (asilimia zaidi ya sita) na Uganda yenye zaidi ya asilimia 43.

Kutokana na takwimu hizo, Serikali za Tanzania, Kenya na Uganda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), chini ya Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), zinatekeleza miradi ya kuimarisha usalama wa usafirishaji salama kwa njia ya maji ndani ya ziwa hilo inayogharimu zaidi ya Sh60 bilioni.

Kwa upande wa Tanzania, miradi hiyo inatekelezwa kupitia Shirika la Uwakala wa Huduma za Meli nchini (Tasac) kwa gharama ya zaidi ya Sh25 bilioni ikihusisha ujenzi wa vituo 10 vya Ufuatiliaji na Uokoaji katika mikoa yote inayopataka na Ziwa Victoria; na tayari ujenzi wa vituo sita tayari umeanza.

Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa Usimamizi wa Usalama, Ulinzi wa mazingira na Usafiri Majini ndani ya Ziwa Victoria uliofanyika mjini Geita Januari 20, 2024, Mratibu wa Kituo cha Utafutaji na Uokokaji Kanda ya Ziwa, Joseph Mkumbo vituo hivyo vinajengwa katika Bandari ya Mwanza Kusini (Mwanza), Musoma mjini (Mara), Kakuru-Nansio (Ukerewe), Kanyara (Buchosa),Chato (Geita) na Bandari ya Bukoba mkoani Kagera.

‘’Pamoja na vifaa vya kisasa vya mawasiliano kwa ajili ya kupokea taarifa za dharura katika ukanda wote wa Kanda ya Ziwa, vituo vya Utafutaji na Uokozi pia vitakuwa na vifaa na vyombo vikiwemo boti za kisasa kwa ajili ya uokozi wakati wa matukio ya dharura,’’ amesema Mkumbo

Katika mahojiano mwishoni mwa mwaka 2023, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Dk Masinde Bwire aliiambia Mwananchi kuwa kwa kutumia namba maalum, vituo vya Utafutaji na Uokozi vitapokea za ajali na matukio mengine ya dharura ndani ya Ziwa Victoria kutegemeana na ukaribu wa kituo na eneo la ajali.

Akizungumzia vituo vya Utafutaji na Uokozi, Dk Bwire anasema yeyote mwenye kuhitaji huduma ya dharura ndani ya Ziwa Victoria atatoa taarifa kupitia namba maalum inayoweza kupokelewa katika kituo chochote ndani ya nchi zote tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.

‘’Taarifa zitapokelewa kutoka Tanzania, Kenya na Uganda na zitafanyiwa kazi kwa haraka na maofisa kutoka kituo cha karibu; lengo kuu ni kuona shughuli ya utafutaji na uokozi wakati wa majanga ya ajali ndani ya Ziwa Victoria zinafanyika kwa haraka,’’ anasema Dk Bwire.

Boti ya Sh4 bilioni kujengwa

Kupitia mikakati hiyo, Serikali tayari imesaini mkataba wa ujenzi wa boti maalum yenye vifaa vya uokozi, huduma za dharura za afya na matibabu kwa gharama ya zaidi ya Sh4 bilioni. Boti hiyo itatoa huduma ndani ya Ziwa Victoria.

Mradi wa ujenzi wa boti hiyo unatekelezwa na kampuni ya Loca Muhendis Link ya Uturuki na ulitiwa jijini Mwanza mwishoni mwa mwaka 2023.

Ajali Ziwa Victoria

Kupinduka na kuzama kwa meli ya MV Bukoba Mei 21, 1996 hatua chache kutoka Bandari ya Mwanza na kupinduka kwa kivuko cha MV Nyerere Septemba 20, 2018 ni miongoni mwa ajali zilizoacha simanzi nchini kutokana na vifo vya watu zaidi ya 1000.

Wakati ajali ya MV Bukoba ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 800, ajali ya MV Nyerere alipoteza maisha ya watu zaidi 225 huku uwezo mdogo wa uokozi ukitajwa kuwa miongoni mwa sababu ya vifo vya watu wengi katika ajali zote mbili.

Utii wa sheria

Ofisa Mfawidhi Tasac Mkoa wa Geita, Godfrey Chegere anasema pamoja na mambo mengine, baadhi ya wamiliki, manahodha wa vyombo na wasafiri kutozingatia sheria ni miongoni mwa sababu zinazochangia siyo tu ajali, bali pia upotevu wa mali na maisha ya watu.

Anasema ili kukabiliana na changamoto hiyo, Tasac kwa kushirikiana na vyombo na mamlaka nyingine za Serikali tunafanya kazi ya kutoa elimu kwa umma kuhusu usafirishaji salama majini na papo hapo kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wakosaji.

‘’Katika usimamizi wa sheria, Tasac imefanya ukaguzi katika mialo ya Mkoa wa Geita ambapo zaidi ya boti 20 wamiliki wake wametozwa faini kati ya Sh250, 000 hadi Sh500, 000 huku vyombo vingine vikifungiwa kwa kukiuka sheria na kanuni za usafirishaji salama majini,’’ anasema Chegere

Ametaja baadhi ya makosa yaliyobainika wakati wa ukaguzi huo kuwa ni abiria kutovaa jaketi okozi, kuzidisha abiria na mizigo ambapo pamoja na faini, wamiliki, manahodha na abiria walipewa elimu kuhusu usafirishaji salama majini.

Mwenyekiti wa Wamiliki wa Boti Mkoa wa Geita, Chaina Kateinawabo ameiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo kuwasaidia wamiliki wa boti za uvuvi na abiria kumudu mabadiliko ya teknolojia na gharama ya kutengeneza boti za kisasa zinazojengwa kwa chuma badala ya zile za asili za mbao.

‘’Pamoja na kuwapunguzia wamiliki gharama ya ukarabati wa mara kwa mara unaotokana na uchakavu wa mbao, ujenzi wa boti za chuma pia utamaliza ajali zinazotokana na boti kuvuja baada ya mbao kuchakaa,’’ anasema Kateinawabo

Chanzo: www.tanzaniaweb.live