Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu 430,000 kunufaika mradi maji Ziwa Victoria

Victoria?fit=700%2C469&ssl=1 Watu 430,000 kunufaika mradi maji Ziwa Victoria

Thu, 16 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Tabora (Tuwasa) ina mpango wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria kwenye miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua na kunufaisha zaidi ya watu 430,000.

Akitoa taarifa ya mradi wa maji wa Ziwa Victoria kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Tuwasa, Mayunga Kashilimu amesema Dola za Marekani 62.2 milioni zitatumika kwenye miji yote mitatu.

Amesema miji hiyo itanufaika kupitia mradi wa miji 28 ambao unagharamiwa na Serikali kupitia fedha za mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya India.

Amesema ujenzi unatekelezwa kwa miezi 36 na umepangwa kukamilika kabla ya mwaka 2025.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji imeiagiza Bodi ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Tabora, Tuwasa, kuhakikisha wanaweka mpango madhubiti wa kuongeza mapato ya mamlaka na kupunguza upotevu wa maji hadi asilimia 20 kutoka asilimia 27.

Wakitoa maazimio ya kamati kupitia mwenyekiti wake, Jerry Silaa amesema lazima upotevu wa maji udhibitiwe na hivyo Tuwasa ifikie asilimia 20 ambayo ndio inaruhusiwa kimataifa.

Kamati pia imeiagiza Bodi ya Tuwasa, kuongeza mkakati wa kukusanya mapato yatokanayo na matumizi ya maji ili iendelee kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wake.

Sanjali na maagizo hayo pia imeiagiza kuwa na utaratibu wa kuonyesha namna mradi ulivyoshiriki kutengeneza ajira kwa wananchi.

Mwenyekiti wa bodi ya Tuwasa, Dick Mlimuka amesema wamepokea maagizo ya kamati na kwamba watayafanyia kazi na kuyatekeleza.

"Tunaishukuru kamati kwa maagizo yake ambayo tumeyapokea na tutayatekeleza".

Chanzo: www.tanzaniaweb.live