Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu 150 wajitolea damu kwenye Maulid Mirerani

52152 Pic+damu

Mon, 15 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mirerani. Katika kuadhimisha miaka 1,440 ya Maulid (mazazi) ya Mtume Muhammad S.A.W, Taasisi ya Masjid Noor ya mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, watu 150 wamepima afya zao na kujitolea damu salama kwa ajili ya wahitaji wa kituo cha afya Mirerani.

Mwenyekiti wa Maulid inayofanyika kwenye taasisi hiyo, Mohamed Issa Mughanja akizungumza leo Jumamosi Aprili 13, 2019 wakati wa upimaji huo na utoaji damu amesema katika sehemu ya maadhimisho hayo wameamua kuchangia damu.

Mughanja amesema kupitia shughuli hiyo ya kujitolea damu salama, damu hiyo itawasaidia wajawazito wanaohitaji kujifungua na kuishiwa damu na watakaopata ajali.

Imamu wa taasisi hiyo, Sheikhe Ramia Isanga amesema katika maadhimisho hayo ya Maulid wameamua kujitolea damu ili kutimiza mafundisho ya Mtume Muhammad S.A.W.

"Katika mafundisho ya Mtume Muhammad S.A.W alituusia kuumika yaani kuchukua, kutoa damu nasi tumefuata mwenendo wake kwa kujitolea damu salama," amesema Sheikh Isanga.

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani, Dk Hassan Ishabailu amesema kabla ya kutoa damu, wanafanya vipimo vya shinikizo la damu, kisukari, ushauri na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU).

Dk Ishabailu amewashukuru wananchi wote waliojitokeza kwenye shughuli hiyo ya kuchangia damu salama ambayo itawasaidia wagonjwa wa kituo hicho cha afya.

Imamu msaidizi wa taasisi ya Masjid Noor, Mohamed Hassan ametoa wito kwa watu kushiriki kwenye kuchangia damu kwani viongozi wote wa taasisi hiyo wamejitolea damu salama wakiongozwa na imamu wao Sheikh Isanga.

Mohamed amesema kupitia maadhimisho hayo wamedhamiria kujitolea damu salama kwenye kituo cha afya Mirerani kwa wahitaji wa sasa na baadaye.

Mmoja kati ya waliojitolea damu salama, Mariam Hassan amesema kutoa huduma hiyo ni jambo zuri kwani unaweza kutoa damu ikakusaidia wewe mwenyewe baadaye au ndugu na jamaa zako.

Mariam amesema anajisikia fahari kujitolea damu salama kwa ajili ya kusaidia wahitaji kwenye kituo cha afya Mirerani na kuwasihi wananchi wengine washiriki hilo.



Chanzo: mwananchi.co.tz