Watu 13 wanahofiwa kufariki dunia huku wengine 14 wakiokolewa baada ya mitumbwi miwili kuzama ndani ya Ziwa Victoria wakati wakitoka kusali ibada ya Jumapili Kijiji cha Ichigondo Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Akizungumza kwa simu nasi leo Jumatatu Julai 31, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amesema tukio hilo lilitokea jana saa 12:30 jioni na tayari mwili wa mtoto anayekadiriwa kuwa na mwaka mmoja umeopolewa.
“Hapa Kijiji cha Igundu kuna kama ras sasa watu walikuwa wakitoka kusali katika kanisa la KTMK ndipo mtumbwi mmoja ukapigwa na dhoruba na kuanza kuzama, ukaja mtumbwi wa pili kwaajili ya kuokoa nao ukapigwa na dhoruba mitumbwi yote miwili ikazama,"amesema Dk Naano
Dk Naano amesema jitihada za kuwatafuta watu hao 13 zinaendelea akidai jana baada ya giza kuingia zoezi la kuwatafuta lilisitishwa.
"Tupo hapa na timu ya usalama ya wilaya tunaendelea kuwatafuta maana jana baada ya giza kuingia hakuna ambacho kingeweza kufanyika ila tu hadi sasa ni mwili mmoja ndio umeopolewa,” amesema
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amekiri kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa zaidi baadaye.
“Ndio nimepokea hizo taarifa na hapa ninajiandaa nielekee huko nadhani nitakuwa kwenye nafasi nzuri kulizungmzia nikishafika eneo la tukio,”amesema Magere