Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto wawili wafariki nyumba ikiungua moto

Moto Watoto Watoto wawili wafariki nyumba ikiungua moto

Mon, 24 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Watoto wawili wamefariki dunia kwa kuungua baada ya nyumba waliyokuwemo kuteketea kwa moto katika Mtaa wa Mfifi, Kata ya Kihesa mkoani Iringa.

Inadaiwa watoto hao, Rehema Masanga (7) na Amos Masanga (5) ambao walikuwa wakiwa wamekumbatiana, walishindwa kujiokoa baada ya mama yao, Skolastika Mgombewa kufunga mlango kwa nje akiwaacha peke yao kisha kuondoka nyumbani.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mafifi, Rabi Mgata amedai kuwa chanzo cha moto huo ni mshumaa ambao ulishika godoro kisha kuunguza nyumba yote.

“Mama yao aliwafungia watoto ndani akaenda kunywa pombe kwa hiyo moto ulivyokuwa unaendelea kuwaka walishindwa kujiokoa, mama alirudi baadaye wakati tayari tumeshazima moto na kugundua watoto wamekufa,” amesema Mgata.

Mgata amesema baada ya kuzima moto walibomoa mlango na kukuta watoto wawili waliokufa huku wakiwa wamekumbatiana kwenye kona moja ya nyumba.

Kwa upande wao baadhi ya majirani wamesema awali walianza kuona moshi ukifuka lakini, wengine walidhani ni wa matairi.

Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Iringa, Isabela Bwago amekiri kuwa chanzo cha tukio hilo ni mshumaa ambao ulishika godoro kisha kuunguza nyumba yote bila kuokoa kitu chochote.

“Ni uzembe wa mzazi ambao aliondoka akiwa amewafungia watoto wake kwa nje. Taarifa ya moto tulipewa kwa kuchelewa na hata ingekuja mapema gari isingeweza kufika eneo la tukio kulingana na miundombinu mibovu,” amesema Bwango.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, Issa Juma amesema wakati majirani wanahangaika kuzima moto huo hawakujua kama ndani kuna watoto.

Ameitaka jamii kuwa kuwa makini na matumizi ya mishumaa, vibatari, taa na kuwa walinzi wa familia zao hasa watoto.

Chanzo: mwanachidigital