Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto wataka ushirikishwaji mipango ya familia

Mon, 13 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kibaha. Umewahi kumshirikisha mwanao katika mambo yako, hususan mipango ya familia? Kama bado, basi watoto wanataka uanze kuwashirikisha.

Wanasema kushindwa kuwashirikisha, kuwasikiliza na kuwapatia taarifa sahihi kuhusu maendeleo na mipango ya familia ni kuwanyima haki yao muhimu.

Ukiwashirikisha, wanasema, miongoni mwa faida watakazozipata ni kujua mipango na namna wazazi na walezi wanavyoendesha familia na kuwaongezea wepesi wa kujieleza wanapokutana na ukatili au mambo yanayowatatiza kwenye makuzi yao.

Watoto wameibua suala hilo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya kufunga miradi ya Shirika la Plan International wilayani Kibaha mkoani Pwani, ambako moja ya miradi iliyoendeshwa kwa miaka 22 ni kuundwa kwa majukwaa yao ili kuijengea jamii nafasi ya kuwasikiliza na kuwashirikisha.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Upendo Robert ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Azimio alisema wazazi wake walianza kumshirikisha baada ya kuamua kuwaeleza faida zake.

“Niliweza kuongea nao kuhusu haki zangu wakaona kumbe naelewa mambo mengi, sasa hivi nashirikishwa,” alisema Upendo ambaye pia ni katibu wa Jukwaa la Watoto wilayani humo.

Pia Soma

Daniel Samweli, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo, alisema mzazi anaweza kupoteza maisha ghafla, akaacha watoto wanahangaika na kushindwa kuendesha maisha yao kwa sababu hakuwashirikisha alipokuwa hai. “Unaweza kufa leo ukawaacha watoto wanahangaika tu wakati kama ungewashirikisha wasingedhulumiwa mali kwa sababu wanajua,” alisema Smweli.

Wazazi, walezi wanasemaje

Ibrahim Issa, mlezi wa watoto waliofiwa na wazazi, alisema kuna faida kubwa kuwashirikisha watoto akisema hakupata shida kujua madeni ya ndugu zao baada ya watoto kueleza kila kitu kwa sababu walikuwa wanashirikishwa katika mipango ya familia.

“Wale watoto walituambia baba yao kabla hajafa aliwaeleza alikopa pesa benki na angemaliza mkopo wake mwakani mwezi wa tisa, watoto wanajua neno siri la simu na kompyuta za baba yao kwa kweli tangu hapo nilijifunza jambo,” alisema Ibrahim.

Alisema kuna faida kubwa kwa wazazi au walezi kuwaeleza watoto mipango yao ikiwamo nyaraka muhimu za mali, ili inapotokea wamefariki ghafla isiwe rahisi kudhulumiwa.

Hata hivyo, Athanasia Joel alisema licha ya watoto kushirikishwa, kuna mambo mengine hahitaji kufanya hivyo.

“Yapo ya kuwashirikisha, lakini siyo kila jambo kufanya hivyo maana wanaweza kurubuniwa nikapoteza mali zangu wakati niko hai,” alisema.

Naye Zuhura Abdalah alisema mzazi anayemshirikisha mwanaye maana yake anamuandaa kuwa mwanajamii mwenye mipango mizuri ya maisha.

“Mnapanga wote mambo ya kijamii na kiuchumi kama kununua kiwanja, kujenga na mingine, ukimwambia kwa nini unakatwa mshahara wako na huna fedha za kutosha utamjenga kuheshimu kidogo kilichopo nyumbani,” alisema.

Kwa upande wake, Innocent John alisema hajawahi kuwashirikisha watoto kwa sababu alijua hawawezi kuchangia katika maendeleo ya familia.

Ofisa tarafa ya Kibaha, Anatory Muhango alisema kila mzazi na mlezi anatakiwa kumshirikisha na kumpatia taarifa sahihi mtoto likiwa ni suala la kisheria.

“Kila mtu anatakiwa kuhakikisha anatunza haki za mtoto, kwa hiyo ushirikishwaji ni haki, wahenga wanasema kuzaa siyo kazi, ila kazi ni kulea, hivyo malezi ya mtoto ndiyo haya tunayowaambia,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz