Bi Stamili Endelea Kaloloma ambae ni kikongwe wa miaka 119, mkazi wa Misegese wilaya ya Malinyi malinyi Mkoa wa Morogoro ametelekezwa na watoto wake watano ambao hawataki kumtunza wala kumpatia mahitaji yake muhimu licha ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na kupewa maagizo ya kumtunza kutokana na uzee wake.
Hali hiyo imemfanya Polisi Kata wa Kata hiyo A/Insp Michael Rasha kuingilia kati na kuona namna ya kumsaidia kikongwe huyo.
Mkaguzi Rasha ameamua kuwaita watoto hao ambao wanaishi maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye Majiji makubwa pamoja na kuwashirikisha Maafisa Ustawi wa Jamii ili kuhakikisha Bi Stamili anapata matunzo pamoja na haki zake za msingi.
Mkaguzi Rasha amesema ni lazima kila mmoja asimame kwenye nafasi yake kwani wazazi wana haki ya kupatiwa huduma zote muhimu kama ambavyo wao walijitoa kuhakikisha watoto wao wanapata mahitaji na kukua kwa afya hadi kufikia hatuabya kwenda kujitegemea wenyewe, Kitendo cha kugomea kumtunza mzazi ni Ukatili lakini pia ni hatari kwa maisha ya mzazi maana kinaweza kupelekea kifo cha mapema.
Majirani wa Kikongwe huyo wamekuwa wakijitahidi kumpa msaada lakini pia kuwasiliana na watoto wa Bibi huyo bila kupata matumaini jambo ambalo liliwafanya wamtafute Polisi anayesimamia Kata hiyo ili kuwatafuta kisheria.