Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto wa mitaani, yatima wazagaa Babati

9daa4972f433699b1dafcc2173f5578d Watoto wa mitaani, yatima wazagaa Babati

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WILAYA ya Babati mkoani Manyara imeshauriwa kuunda sheria ndogo ili kukabili ongezeko la watoto yatima na wa mitaani.

Shirika la Tanzania Child and Youth Rescue Organization (TCYRO) limeishauri halmashauri ya wilaya hiyo kuunda sheria hizo ili kuwabana wazazi wanaoshindwa kutekeleza wajibu na kuwaacha watoto hao wakizagaa kwa wingi mitaani bila ya kuwahudumia.

Mkurugenzi Mkuu wa TCYRO, Oscar Daniel alitoa rai hiyo wakati akikabidhi misaada ya vyakula, vinywaji na nguo kwenye kituo cha kulea watoto yatima cha Mahoce kilichopo Babati, mkoani Manyara.

“Wapo watoto wengi yatima ambao wazazi wao wamefariki dunia lakini wana ndugu wasiochuka jukumu la kuwasaidia, lakini pia kutengana kwa wazazi kunakowafanya kila upande kususa kutoa matunzo na mahitaji ya watoto kunasababisha waishi bila kupata mahitaji na ulinzi wa wazazi wao.”

"Kwa hali hiyo tunatarajia kuanzisha mradi hapa Manyara ambao pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu wazazi kuzingatia majukumu na wajibu wao katika kuwahudumia na kulinda watoto wao, lakini pia tutafanya ushawishi kwa halmashauri kukazia sheria zilizopo ili kuunda sheria ndogo ambazo zitawabana wazazi kuhakikisha wanawahudumia, kuwalinda na kuwatunza watoto wao," alisema.

Daniel alisema shirika hilo pia linatoa elimu ya afya ya uzazi kwa jamii ili kuwapa mwanga wa stadi za maisha na afya ya uzazi, malezi na matunzo ya watoto.

Mwalimu mlezi wa kituo hicho alisema pamoja na kupokea misaada mbalimbali kutoka kwa watu wanaoguswa na watoto hao, bado mahitaji kwa ajili ya kuwahudumia watoto ni mengi kutokana na misaada kupungua.

“Wapo watoto yatima wasio na wazazi lakini pia tumekuwa tukihudumia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu ambao wamekimbiwa na wazazi wao na kuachiwa nyumba hivyo kula, kuishi kwao kunakuwa kugumu na wengine kujiingiza kwenye vitendo viovu,” alisema.

Baadhi ya watoto waliozungumza baada ya kupokea msaada huo walilishukuru shirika la TCYRO kwa misaada waliyotoa na kueleza kwamba itawawezesha nao kusherehekea vizuri sikukuu za mwisho wa mwaka kama watoto wengine. Mmoja wa watoto hao, Clara Francis ambaye amefiwa na mzazi mmoja alisema amelazimika kuishi kituoni hapo kwa kuwa mama yake mzazi hana uwezo wa kumhudumia na maisha ya nyumbani kwao ni magumu.

Chanzo: habarileo.co.tz