Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto tisa wa familia moja waungua Musoma, mmoja afariki

MOTO WATOTOFAMILOIA Watoto tisa wa familia moja waungua Musoma, mmoja afariki

Mon, 7 Nov 2022 Chanzo: mwanachidigital

Mtoto mmoja amefariki dunia na wengine wanane kujeruhiwa baada ya nyumba walimokuwa wamelala kushika moto katika mtaa wa Buhare Mjini Musoma.

Moto huo ulizuka usiku wa kuamkia Novemba 5, 2022 na kuunguza watoto hao tisa wa familia moja ambapo mmoja alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.

Watoto watatu kati ya wanane hali zao ni mbaya ambapo wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumatatu Novemba 7, 2022, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema kuwa chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana.

"Ni kweli tukio limetokea, mtoto mmoja amefariki na wengine watatu hali zao ni mbaya, tayari tumeanza uchunguzi tutatoa taarifa kamili baada ya kukamilisha uchunguzi wetu " amesema Magere kwa njia ya simu.

Hata hivyo, baba mzazi wa watoto hao, Emmanuel Magiri amesema kuwa tukio hilo lililotokea baada ya umeme kukatika ndipo watoto hao waliokuwa wamelala pamoja kwenye chumba kimoja kuamua kuwasha mshumaa kwaajili ya kupata mwanga.

"Baada ya kuwasha mshumaa walipitiwa na usinguzi ndipo godoro walilokuwa wamelalia likashika moto na kusambaa chumba kizima" amesema

Magiri amesema kuwa akiwa amelala kwenye nyumba ya pili alisikia kelele za watoto kuomba msaada na alipotoka nje alikuta tayari chumba cha watoto kimeshika moto.

Amesema baada ya kuona chumba hicho kimeshika moto, alisaidiana na majirani kuwaokoa kutoka kwenye moto na kuwapeleka hospitali.

Daktari aliyewapokea watoto hao katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dk Charles Paschal amesema kuwa baada ya watoto hao kupokelewa walipewa huduma ya kwanza lakini mmoja alifariki dunia akiwa anaendelea na matibabu hospitalini hapo.

"Bahati mbaya jana mmoja wa majeruhi alifariki dunia kwasababu ya kiwango cha kuungua kilikuwa kikubwa zaidi kwenye mwili wake, wengine watatu hali zao ni mbaya huku wengine watano wanaendelea vizuri" amesema kwa njia ya simu

Dk Paschal amemtaja mtoto aliyefariki kuwa ni Paschal Emanuel (10) na wengine waliojeruhiwa ni pamoja na Dotto Emanue (6), Benson Emanuel (6), Asteria Emanuel (2), Kulwa Magiri (3) pamoja na pacha wake Dotto Emanuel.

Wengine ni Asteria Emanuel (11), Cecilia Emanuel (3) na Brighton Dotto Emanuel.

Chanzo: mwanachidigital