Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto 22, 000 waondolewa kwenye utumikishwaji

Child Labour Watoto 22, 000 waondolewa kwenye utumikishwaji

Mon, 18 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watoto zaidi ya 22,000 wenye miaka kati ya mitano hadi 17 wameondolewa kwenye kazi za utumikishwaji zikiwemo za mashamba ya tumbaku katika halmashauri tano za Chunya, Songwe, Kaliua, Urambo na Sikonge mkoani Mbeya, Songwe na Tabora katika kipindi cha miaka 11 iliyopita.

Meneja Mradi wa Prosper Reset unaojishughulisha na kuwaondoa watoto katika utumikishwaji, Fred Malaso ameeleza hayo Septemba 16, 2023 katika kikao cha kufuatilia mfumo wa masuala ya utumikishwaji watoto kilichohudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka vyama vya wafanyakazi, Chama cha Waajiri nchini, (ATE), wanunuzi wa tumbaku, maafisa ustawi na maendeleo ya Jamii wa halmashauri.

Malaso amesema watoto hao wamesaidiwa kwa kupelekwa shule pamoja na kupewa stadi za maisha, kufundishwa ufundi wa aina mbalimbali ukiwemo ujenzi, ushonaji, uashi ambazo zimewasaidia kuingiza kipato na kuachana na utumikishwaji.

“Hatukuwaacha pasipo kuwapa kitu cha ziada na ndio maana tumewapa ujuzi unaowasaidia huku wengine tukiwapeleka shuleni”amesema

Amesema wazazi na walezi wa watoto wanaosoma shule walipewa elimu ya ujasiriamali na kuanzisha vikundi 50 vyenye mitaji ya zaidi ya Sh180 milioni ambayo inakua na kuwasaidia.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Leonard Celestine amesema yawepo mazingira ya kazi yasiyohusisha mtoto ambayo yatakuwa na staha kwake.

“Lazima tupinge utumikishwaji watoto katika maeneo ya kazi na kutomhusisha mtoto kabisa,”amesema

Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Suzan Mkangwa mbali na kupongeza ushirikiano wa wadau katika kupiga vita utumikishwaji watoto ,ametaka ushirikiano wa wadau wote kutokomeza ajira kwa watoto.

“Tunapongeza ushirikiano wa wadau wote na lengo letu liwe ni kutokomeza utumikishwaji watoto ambalo ndio lengo la Serikali,”amesema

Malengo ya kikao hicho ni kufuatilia mfumo wa masuala ya utumikishwaji watoto na kujadili namna bora zaidi ya kufuatilia masuala ya utumikishwaji watoto na upatikanaji wa taarifa kutoka ngazi za jamii.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live