Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoa darasa la wasichana kujitambua shuleni

48696 Darsa+pic

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wafanyakazi wanawake kutoka Taasisi ya Haki elimu wamewafunda wanafunzi wa kike wa shule za sekondari Jangwani na Tambaza, wakiwataka wasijiingize kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Walisema uhusiano huo utawapotezea ndoto zao kielimu, kutokana na kupata mimba suala linaloweza kuepukika.

Akizungumza katika mdahalo uliowakutanisha wafanyakazi hao na wanafunzi kuadhimisha wiki ya wanawake duniani, Ofisa programu wa Haki Elimu, Rose Kalage alisema kiuhalisia mimba za utotoni ndio chanzo kikubwa cha ndoa za utotoni.

“Ukishapata mimba wazazi wataona bora mmalizane na kwa kuficha aibu utaozeshwa, kwa hiyo jitunzeni, semeni hapana na msikubali kabisa kupoteza ndoto zenu kizembe,” alisisitiza.

Mfanyakazi mwingine Lilyan Omary aliwataka wasichana kujiwekea malengo yao na kutumia muda mwingi kujiuliza wapo shuleni kufanya nini.

Alisema jibu la swali hilo ndilo litakalowapa nguvu ya kufanya vizuri zaidi darasani.

“Tumieni hata wanawake waliofanikiwa kujilinganisha nao, unaweza kutaka kuwa kama Jocate Mwigelo (Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe) basi tulia ujifunze alifanyaje? alisomaje? ilikuwaje? Ukifanya hivyo utafika mbali sana,” alisema Lilyan.

Alisema hakuna maisha ya mkato na wakitaka maisha hayo kwa sababu ya tamaa itakuwa vigumu kufikia Tanzania ya viwanda inayohubiriwa kwa sababu wataishia njiani kielimu.

Aliwataka kujifunza na kushiriki katika midahalo mbalimbali ya kimafunzo shuleni bila kusahau michezo inayoweza kuiweka vizuri miili yao.

Awali baadhi ya wanafunzi walisema tamaa za fedha na zawadi ndogo ndogo ndizo ambazo huwaponza wenzao na kujikuta wakiacha masomo kwa kupata mimba.

Mwanafunzi Magdalena Makungu kutoka Shule ya Sekondari ya Jangwani alisema wasichana wengi wanahitaji elimu ya afya na kujitambua ili waweze kupambana na vishawishi.

“Madhara ya mimba ni mengi , mimba inaweza kusababisha vifo, umaskini, watoto wa mtaani na mengine mengi, tunaweza kujikinga lakini tunahitaji elimu zaidi hasa ya kujitambua,” alisisitiza.



Chanzo: mwananchi.co.tz