Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watendaji wa mitaa kusimamia ujenzi

Watendaji wa mitaa kusimamia ujenzi

Thu, 14 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wizara ya Ardhi imepanga kuwapa barua watendaji wa vijiji na mitaa ili wawe kama watumishi wa Wizara hiyo wakiwa na jukumu la kusimamia ujenzi katika maeneo yao ili kuepuka watu kujenga kinyemela.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, William Lukuvi ametoa kauli hiyo leo Jumapili Novemba 10, 2019 Jijini Dodoma alipotembelea eneo la mgogoro wa ardhi ya Nzuguni na kupiga  marufuku ujenzi usiofuata taratibu kuanzia vijijini na hata mijini.

Waziri Lukuvi amesema maofisa ardhi ni wachache ambao hawawezi kufika katika kila kipande cha ardhi ya Tanzania ambacho kinafanyiwa maendelezo lakini kwa kuwatumia maofisa watendaji wa maeneo hayo hakuna kitakachoshindikana.

Amesema utaratibu wa sasa ambao watu wanautumia wa kupata viwanja na kuanza kujenga hauna budi kuachwa mara moja kwani hata katika maeneo ya vijijini watu wanatakiwa kujenga kwa utaratibu ili kusaidia hata upitishaji magari nyakati za hatari.

“Kuanzia sasa nitatoa barua za kuwatambua maofisa watendaji katika maeneo yao ili wa mjini awe kama ofisa mipango miji na wa vijijini wawe maofisa ardhi na watakuwa na mamlaka ya kusimamia vibali vya ujenzi vyote ikiwemo kuwapa elimu watu wa vijijini namna bora ya kujenga na aina ya majengo katika mitaa yao,” alisema Lukuvi.

Hata hivyo Waziri huyo amerudia kauli yake kuwa, katika maeneo ambayo upimaji na utambulizi ulishafanyika hayaruhusiwi kuvunjwa badala yake watu wapewe elimu namna ya kuboresha makazi yao kwani lengo la serikali ni kila mtu apate uhalali wa kumiliki eneo lake na kulilipia kodi.

Amesema watu waliojenga tangu mwanzo na ambao miundombinu itakuwa imepitia katika maeneo yao, hao ndiyo watazungumza nao na kuona jinsi ya kufanya.

Akiwa eneo la Nzuguni Waziri Lukuvi alishuhudia utapeli uliofanywa na baadhi ya watu kwa kuziuzia ardhi kampuni hewa wakiwamo wabunge ambao aliwaomba kuwa watulivu ili Serikali ione namna bora zaidi ya kumaliza mgogoro.

Chanzo: mwananchi.co.tz