Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watendaji kata Mbeya wakabidhiwa pikipiki

45bef62f5fe69c5419df1377806ec4d8.jpeg Watendaji kata Mbeya wakabidhiwa pikipiki

Tue, 20 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya imekabidhi pikipiki 12 zenye thamani ya Sh milioni 33 kwa maofisa watendaji wa kata kwa lengo la kuongeza ufanisi kazini kwa kuwarahisishia kufika kwa wakati mahali wanapohitajika.

Wazo la halmashauri la kununua pikipiki kwa maofisa watendaji ni sehemu ya kuunga mkono mpango wa serikali wa kuanza kutoa Sh 100,000 kwa kila ofisa mtendaji wa kata kwa kila mwezi kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022.

Akizungumza wakati wa kugawa pikipiki hizo juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Stephen Katemba alisema pikipiki hizo 12 zimenunuliwa kwa awamu ya kwanza na awamu itakayofuata itakuwa kukamilisha kwa kata 16 zilizosalia.

Alisema kipaumbele cha halmashauri hiyo kwa mwaka huu wa fedha ni kuhakikisha watumishi wanatengenezewa mazingira bora ya kufanyia kazi na kuwafanya kuondokana na manung'uniko kazini.

“Tulianza na kipaumbele cha kuhakikisha makusanyo yetu yanakwenda kama tunavyopanga...katika hilo tumefanikisha kwa asilimia 100 na sasa hiyo itabakia kuwa kawaida yetu. Lakini huwezi ukawa unakusanya makusanyo wakati wanaokusaidia kukusanya wanalia, ndiyo maana kipaumbele chetu mwaka huu itakuwa kuhakikisha rasilimali watu inakuwa yenye furaha,” alisema.

Ofisa Utumishi wa Wilaya ya Mbeya, Nicodemus Tindwa aliwataka maofisa watendaji waliokabidhiwa pikipiki hizo kuzitumia kwa matumizi ya ofisi pekee na si shughuli binafsi zinazoweza kuwasababishia wadau kuanza kuwajadili.

Chanzo: www.habarileo.co.tz