Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu wafa kwa kupigwa na radi

3cb21b0f899af7ceae229238eefc4a51 Watatu wafa kwa kupigwa na radi

Fri, 8 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKAZI watatu wa Kijiji cha Kitahana Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, wamekufa kwa kupigwa na radi kutokana na mvua kubwa.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibondo, Ayoub Sebabili alisema tukio hilo ni la juzi asubuhi. Alisema kwamba mtu mmoja, kati ya hao watatu, ametambuliwa. Mwili wake umechukuliwa na ndugu kwa mazishi.

Sebabili alisema kuwa watu wawili, bado hawajatambuliwa na maiti zao zimehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo.

Katika tukio lingine, watu kutoka familia 33 katika Kijiji cha Kibingo Wilaya ya Kibondo, hawana makazi baada ya nyumba zao kubomoka kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na mawe. Mvua hiyo pia ilijeruhi watu watatu.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo la tukio, Katibu Tawala Wilaya Kibondo, Ayubu Sebabili alisema wilaya inahitaji msaada wa haraka wa mavazi na chakula, ili kuwasaidia wahanga. Alisema tayari kamati ya maafa ya wilaya, imeanza kupokea misaada kutoka wadau mbalimbali.

Mwenyekiti wa Kijiji Cha Kibingo, Mawazo Gwahiye alisema mvua hiyo ilinyesha kwa dakika kumi na tano na kuleta uharibifu mkubwa wa mali na nyumba.

Alieleza kuwa mashamba yameharibika, mazao yamesombwa na nyumba zimebomoka, hali ambayo imewaacha watu wengi katika hali mbaya ya ukosefu wa huduma za msingi.

Mmoja wa wahanga, Leonia Marco alisema tukio hilo lilipotokea, walikuwa shambani na walipofika nyumbani walikuta nyumba imebomoka, lakini watoto wapo salama. Alisema watoto hao waliokolewa na majirani.

Kufuatia hali hiyo, Shirika la Caritas Kigoma limetoa msaada wa nguo belo saba ikiwemo mablanketi, mashuka, mafuta ya kupaka na chakula.

Mkurugenzi wa Caritas Kigoma, Benedict Gwimo alisema baada ya tukio hilo, walipata maombi kutoka kwa kamati ya maafa ya wilaya,na kushauriana kwa haraka na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma, Joseph Mlola na kuamua kutoa msaada huo.

Alisema Caritas itaendelea kusaidia waathirika hao kadri mahitaji yatakavyokuwa. Alisema kwamba kitendo hicho ni cha utu.

Chanzo: habarileo.co.tz