Watu watatu Mkoa wa Mwanza Wilayani Misungwi wanashikiliwa na Vyombo Ulinzi kwa tuhuma za kuiba Ng'ombe katika Shamba la Serikali la Mabuki ambalo limetolewa kwa ajili ya Mradi wa vituo kwa vijana waliosomea Mifugo waweze kujiajiri.
Katika watu hao pia yuko mfanyakazi katika shamba hilo Daudi Msobi anayedaiwa kushirikiana na watuhumiwa wengine wawili kuiba ng'ombe sita.
Baada ya watuhumiwa kuiba ng’ombe hao waliwatoa hereni walizowekewa masikioni na kuzitupa ili kupoteza ushahidi kisha kwenda kuwauza Kata ya Misasi ndipo wakakamatwa.
Meneja wa Kampasi ya Mabuki, Jacob Ngowi amesema ng'ombe hao huesabiwa pindi wanapotoka kwenda malishoni na wanaporudi na baada ya kuhisi kuwepo kwa wizi huo wakazidisha umakini katika kuwahesabu na kubaini upotevu wa ng'ombe hao.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, Poul Chacha amesema walilibaini hilo mapema ndipo wakakweka mtego na kufanikiwa kuwatia mbaroni watu hao huku akiwaonya wengine watakaojaribu kujihusisha na wizi wa ng'ombe hao au kufanya uhalifu wowote.