Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu (majina yanahifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi) wakazi wa Tunduma kwa tuhuma za kuingiza nchini vipodozi vya aina mbalimbali vilivyopigwa marufuku vyenye viambata sumu pamoja na bidhaa za magendo kupitia njia za panya.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, ACP Benjamin Kuzaga amesema watuhumiwa wamekamatwa Machi 03, 2023 majira ya saa 12:30 asubuhi katika misako iliyofanyika maeneo ya Izumbwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini na kufanikiwa kuwakuta wakiwa na vipodozi vya aina mbalimbali vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku nchini ambavyo ni:-
-CARORITE BOX 20 -CREAM AINA YA NAOMI CATON 10 -NEPROSONE GEL BOX 45 -CREAM PEAU CREIRE CATON 8. -DIANA CATON LOTION 8, -CREIRE FOR MEN CATON 12. -DERMO GEL DAZAN 26, -COCOPUP BOX 26 -MAFUTA AINA COCOPAP BOX 04. -EPIDERM ZIPO CATON 9. -VAROLIGHT BOX 2. -BETASOL BOX 2. -DERMO GEL 26
Ameongeza kuwa katika upekuzi, watuhumiwa walikutwa na mali Vitenge jola 26 vilivyoingizwa nchini bila kulipiwa ushuru wa forodha kupitia njia zisizo rasmi vikiwa ndani ya Gari namba T.165 BQT aina ya Cresta GX 100.
Watuhumiwa walikuwa wakisafirisha vipodozi hivyo vyenye viambata sumu na Vitenge hivyo kwa kutumia gari yenye namba za usajili T.165 BQT CRESTA GX 100 kutoka nchini Zambia kupitia njia isiyo rasmi ya Ilembo Umalila.
Kamanda Kuzaga amesema watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.