Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watano wafariki mafuriko Morogoro

Mvua Mvua Kifo.png Watano wafariki mafuriko Morogoro

Fri, 26 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu watano wamepoteza maisha baada ya kusombwa na maji yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika eneo Kihonda kwa Chambo.

Mvua hiyo iliyoanza jana ilisababisha mji wa Morogoro kufurika maji ndani ya muda mfupi, kiasi cha watu kushindwa kuendelea na shughuli za kila siku.

Kufuatia maafa hayo, askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi Tanzania na Jeshi la Magereza Tanzania mkoani Morogoro, wameshiriki katika uokozi wa wananchi waliozingirwa na maji katika maeneo ya Kihonda Mbuyuni, Kihonda Manyuki na Lukobe.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Januari 26, 2024 mjini hapa, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Rajabu Marugujo amesema watu watano wamefariki, huku 246 wakiokolewa baada ya kuzingirwa na maji.

Kamanda Marugujo amesema kati ya waliofariki, mtu mmoja ndiye aliyetambuliwa kwa jina la Omari Juma (20) baada ya mwili wake kuopolewa katika eneo la Kihonda kwa Chambo, huku miili mingine ikiwa bado haijatambuliwa.

“Maji yalizingira kaya 157 kutokana na mvua zilizoanza kunyesha saa 6 mchana katika maeneo mbalimbali mkoani hapa, hata hivyo tulifanikiwa kuokoa watu 246 waliokuwa wamezingirwa na maji hayo.

“Katika eneo la Kihonda kwa Chambo watu watano wamesombwa na maji na kupoteza maisha na nyumba nyingi zimebomoka na kuanguka katika kata ya Lukobe, Kihonda na maeneo mengine,” amesema Kamanda Marugujo.

Mkazi wa Kihonda, Barabara ya Mazimbu, Zakaria Issaya amesema mafuriko yamesababisha watu kuhama makazi yao.

“Serikali iwe na utaratibu wa kuchunguza haya mafuriko na madhara yake kwa wananchi kwa sababu haya si ya kwanza kutokea na kuleta madhara,” amesema Zakaria.

Naye Steven Maliki amesema ameshuhudia mtu aliyekuwa akiendesha gari akisombwa na kupoteza maisha kutokana na maji kuwa na nguvu.

“Hatari ni pale mtu anapoona anaweza kuvuka maji kwa miguu, baiskeli, pikipiki au gari, lakini matokeo yake maji yanamsomba na kumsababishia umauti au aokolewe kama kutakuwa na watu walioona tukio,” amesema Maliki.

Akizungumzia maafa hayo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amewataka wananchi kuacha kung’ang’ania kukaa maeneo yenye hatari hata baada ya kuvamiwa na maji.

“Unapoona hatari kwa maji kuvamia makazi yako, kitu cha msingi hapo ni kuondoka na kwenda eneo salama utakuwa umeokoa maisha yako badala ya kung’ang’ania, athari yake ni kubwaikiwamo kupoteza maisha, tuchukua hatua ya kujiokoa,” amesema Malima.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live