Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watano wafariki kwa mafuriko Moshi

Watano Wafariki Kwa Mafuriko Moshi Watano wafariki kwa mafuriko Moshi

Thu, 25 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu watano wamefariki dunia wakiwemo Watoto watatu wa familia moja, huku kadhaa wakijeruhiwa, kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.

Pamoja na vifo hivyo, nyumba kadhaa zimeanguka na nyingine kuzingirwa na maji na kusababisha kaya kadhaa kukosa makazi huku mifugo, vyakula na mali nyingine, vikisombwa na maji hayo ya mafuriko katika Kata za Mji Mpya, Msaranga, Kimochi, Kahe na Mabogini wilayani humo.

Mafuriko hayo ambayo yametoka usiku wa kuamkia leo Aprili 25,2024, yanatokana na mto Rau kujaa maji na kuvunja Kingo za mto huo na kupelekea maji kutapakaa katika maeneo ya makazi ya watu na mashamba na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na vifo.

Akizungumza wakati wa uokozi katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema mafuriko hayo yametokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani hapo.

"Vifo vitatu ambavyo ni vya watoto vimetokea kata ya Kimochi baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuangukiwa na kifusi, ambao watu wanne katika familia hiyo wamejeruhiwa na tumewakimbiza katika hospitali ya Mawezi, lakini miili mingine miwili tumeiopoa eneo la Msaranga na msitu wa Rau, ambayo ilikuwa imesombwa na maji," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live