Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watakiwa kushirikiana kugawa maeneo ya kiutawala

A079f6b02d0a659fe5f2ae0d7b469180 Watakiwa kushirikiana kugawa maeneo ya kiutawala

Tue, 23 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

HALMASHAURI za Jiji la Mbeya na ya Wilaya ya Mbeya zimeshauriwa kuwa na mikakati shirikishi katika uainishaji wa mapendekezo ya kuyagawa maeneo ya kiutawala.

Hali hiyo imeelezwa inatokana na ukweli kuwa upo uwezekano mkubwa wa baadhi ya maeneo kutakiwa kuhamishwa kutoka eneo moja la kiutawala kwenda jingine .

Katibu Tawala , Saitoti Zelothe alitoa ushauri huo alipozungumza na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya walipojadili mapendekezo ya kuigawa halmashauri hiyo pamoja na wilaya, ikiwa ni kutekeleza agizo la ahadi aliyoitoa Rais John Magufuli wakati wa kampeni za mwaka jana.

Zelothe alisema kwa kuwa lengo la rais ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki za kiutawala kwa urahisi ni muhimu jiografia rafiki ikazingatiwa wakati wa ugawaji wa maeneo ya kiutawala ili matokeo ya mgawanyo huo yawe yenye tija na si yenye kuzua malumbano wala malalamiko ndani ya jamii.

"Rais alitoa ahadi kwa upande wa Halmashauri ya jiji la Mbeya na Halmashauri ya wilaya ya Mbeya.Kwenye mchakato wa aina hii ni vizuri hizi halmashauri zetu zote mbili zikakaa kwa pamoja zikaona ni namna gani nzuri zaidi ya kama kufanya ugawaji hata wa hizi kata.

Mnaweza mkakuta kuna baadhi ya kata zinaweza kuwa na tija zaidi kwa wananchi kama zitakwenda kwenye Halmashauri ya jiji la Mbeya. Na kuna baadhi ya kata mkaona zinaweza kuwa na tija zaidi zikitoka jiji kuja halmashauri ya wilaya ya Mbeya," alisisitiza.

Alisema kutokana na hali hiyo ni vizuri wataalamu wa pande zote mbili kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu tawala huyo kukutana kwa pamoja huku akisema kwa upande wa Halmashauri ya jiji la Mbeya tayari kuna mazungumzo yameanza.

Alisema ni jambo jema vitu kama hivyo vikafanyika kwa ushirikiano wa pamoja ili isitokee baadaye mapendekezo yanafanyika na kupelekwa mbele yakakwama kwa sababu hazikufanyika mbinu zenye kuonesha manufaa ya pande zote kwa maslahi ya wananchi.

Kwa upande wao madiwani kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Ezekia Shitindi walisema ugawaji wa maeneo ya kiutawala ni muhimu ukazingatia matakwa ya wananchi na si maslahi ya viongozi wachache wenye kulenga kujinufaisha kisiasa.

Chanzo: habarileo.co.tz