Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watakiwa kuondoka shamba aliloanzisha Nyerere Chamwino

1f064620484f26f0de783a08947bb798.jpeg Watakiwa kuondoka shamba aliloanzisha Nyerere Chamwino

Sat, 2 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imeagiza wananchi waliovamia eneo liitwalo Farm katika kijiji cha Chamwino Ikulu, mkoani Dodoma kuondoka katika kipindi cha wiki mbili kuanzia leo, kwa kuwa lilishatangazwa kuwa eneo la umma lenye matumizi tofauti.

Hatua hiyo inaelezwa ilifikiwa mwaka 1992 kupitia Gazeti la Serikali Na 263 la Juni 25, 1992 ili kuepusha Sheria ya Ardhi ya Vijiji (Sura 114 Toleo la 2002) kutumika.

Agizo la kuwaondoa wavamizi hao lilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Gift Msuya wakati akitangaza maamuzi ya timu ya uchunguzi wa mgogoro wa eneo la shamba hilo mbele ya wananchi wa kijiji cha Chamwino.

“Natoa tamko la Serikali kwa niaba ya kamati ya ulinzi ya wilaya na wananchi wa kijiji cha Chamwino. Naagiza wanaokalia maeneo ndani ya eneo la Farm kuondoka ndani ya wiki mbili na watakaokaidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Msuya.

Sehemu ya eneo la shamba la Farm lenye ukubwa wa ekari 640 lilianzishwa kati ya mwaka 1971/1972 na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo la kuwafunza wanakijiji wa Chamwino ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi, kondoo, nguruwe na kuku.

Hata hivyo, limevamiwa na kuzua mgogoro kati ya wananchi na serikali. Kwa mujibu wa Msuya mwananchi yeyote aliyeingia ndani ya eneo hilo ni marufuku kufanya shughuli yoyote kama vile ujenzi, kilimo na kwamba serikali kupitia idara ya ardhi itaweka mabango katika eneo hilo kuonesha kuwa hilo ni eneo la umma.

“Wanaoendelea kufanya ujenzi watakuwa wanajiingiza hasara na mwananchi yeyote mwenye nyaraka za kumilikishwa sehemu ya eneo hilo la Farm afike ofisi ya Mkuu wa Wilaya na atapatiwa haki yake,” alisema.

Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi nchini, Nathaniel Nhonge alisema kumbukumbu katika eneo hilo zimeweka bayana kuwa eneo lenye mgogoro la Farm lilitolewa kwa matumizi ya umma na hakuna mabadiliko yaliyofanyika kwenda kwa mtu mmoja mmoja.

“Kimsingi hakuna mtu aliyelipwa fidia ndani ya eneo la Farm na wale wananchi waliolipwa kimakosa wanatakiwa warejeshe fedha,” alisema.

Nhonge alisema baada ya ripoti ya Tume ya Uchunguzi kuhusiana na mgogoro huo sasa upimaji utafanyika ili eneo lililotolewa kwa matumizi ya taasisi za umma kama Shule ya Sekondari Chamwino, Shule ya Msingi Kikwete pamoja na eneo la mahakama, yamilikishwe kwa wahusika ili kuepuka migogoro hapo baadaye.

“Serikali itaweka utaratibu wa kudumu wa kubaini na kulinda maeneo mengine ya aina hii yaliyoko ndani ya Chamwino dhidi ya uvamizi wa wananchi,” alisema Nhonge.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa kijiji cha Chamwino wameonesha kutoridhishwa na maamuzi hayo kwa kueleza kuwa maeneo hayo walirithi na kuridhiwa na serikali ya kijiji kwa nyakati tofauti ingawa hawakuwa na nyaraka zozote zinazoonesha kumilikishwa maeneo hayo.

Eneo la Farm katika kijiji cha Chamwino mkoani Dodoma limekuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu uliosababisha kuundwa kwa timu maalumu ya kushughulikia mgogoro huo. Wakati wa kushughulikia mgogoro, timu ya uchunguzi ilielezwa kuwa, shamba la Farm lilitolewa kwa serikali ya kijiji miaka ya 1971/1972 kwa matumizi ya mradi wa mifugo na baada ya mradi kufa mwaka 1995 baadhi ya wananchi waliokuwa eneo hilo kabla ya Farm kuanzishwa walirudi kwenye eneo hilo na wengine waliomba serikali ya kijiji kwa ajili ya kulima mashamba kwa muda.

Inaelezwa kwamba serikali ya kijiji cha Chamwino ilitoa sehemu ya eneo hilo kujengwa Shule ya Sekondari ya Chanwino mwaka 1995 na sehemu ya shamba hilo lililotolewa kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi ya Kikwete 2007.

Sheria ya Ardhi ya Kijiji Na 4/1999 kifungu cha 13 (7) inaeleza kuwa ardhi iliyotengwa na halmashauri ya kijiji au mkutano wa kijiji kwa matumizi ya jumuiya/umma au ardhi ambayo wenyeji wa eneo husika wanaitumia kama ardhi ya kijiji ya umma kabla ya kutungwa kwa sheria ya ardhi, ardhi hiyo ni ya kijiji.

Pia sheria ya ardhi ya mwaka 1999 kifungu cha 12 (1) inakataza ardhi ya jumla kutolewa kwa mtu binafsi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz