Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watakiwa kuondoa vibanda maeneo yote yasiyo rasmi

8a09fa8936c51e52069684575442e90f Watakiwa kuondoa vibanda maeneo yote yasiyo rasmi

Thu, 12 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imewaagiza wafanyabiashara wote waliojenga vibanda maeneo yasiyo rasmi yanayotumika na wapita njia pembezoni na barabara kuondoa vibanda hivyo mara moja.

Aidha wale waliojenga vibanda hivyo pembezoni mwa majengo ya ofisi wanatakiwa kuondoa kwa kuwa siyo rasmi kwa ajili ya kufanya biashara.

Ofisa Masoko wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, James Yuna alisema hayo alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara waliovamia na kuweka biashara zao kwenye barabara zinazotumiwa na watembea kwa miguu na kusababisha usalama kuwa mdogo.

Alisema agizo hilo ni pamoja na wale wote walioweka meza zao za biashara pembezoni mwa majengo mbalimbali ya ofisi kwa kuwa wamekuwa wakileta usumbufu kwa watumishi.

Alisema maeneo hayo yanatakiwa kuachwa wazi kwa kuwa hayako raami na pia siyo salama kwa kufanya biashara ukizingatia kuwa yanahatarisha maisha yao na hata kwa bidhaa wanazozipanga.

Alisema kuna makundi ya wafanyabiashara wamevamia maeneo yasiyo rasmi na kukiuka kanuni, sheria na utaratibu wa halmashauri ya jiji ambapo wameamua wao wenyewe kuweka biashara bila kujali usalama huku wakitambua kuwa kufanya hivyo ni makosa, pia ni hatari kwa kuwa hawaruhusiwi.

"Hivyo halmashauri ya jiji inawataka muache wazi maeneo haya ya barabara na yanayotumika na watembea kwa miguu na hata kwa wale walioweka meza pembezoni mwa majengo ya ofisi ninataka yawe wazi kwa usalama wenu,"alisema.

Aidha amewataka wafanyabiashara hao kutotumia vitambulisho kama sehemu ya kuvunja sheria kwa kufanya biashara maeneo yoyote bila kujali maelekezo yanayotolewa na Halmashauri ya Jiji.

Alisema vitambulisho hivyo pamoja na kuwafanya wawe huru, wanatakiwa pia kutii sheria na maelekezo ambayo yanayowataka kufuata kanuni na sheria ukizingatia kuwa wao ni wadau wa Halmashauri ya Jiji.

Chanzo: habarileo.co.tz