Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watakiwa kufanya shughuli za uvuvi kisheria

180c46549f0a4bca9428f01979e5c02a.jpeg Watakiwa kufanya shughuli za uvuvi kisheria

Sun, 16 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAVUVI nchini wametakiwa kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ili rasilimali hizo ziwasaidie kujiingizia kipato na kujijenga kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Emmanuel Bulayi katika warsha ya kuwajengea wavuvi na wadau wengine uwezo kuendeleza rasilimali za uvuvi.

Alisema serikali inawataka wajasiriamali wa uvuvi kutumia kwa weledi rasilimali za uvuvi zilizopo nchini, ikiwemo kuvua kwa tija ili kusaidia sekta ya uvuvi kuchangia pato lao na la taifa.

“Tunafahamu jamii inayoishi karibu na rasilimali za uvuvi inategemea biashara hiyo, nawaomba baada ya warsha hii muende kutoa elimu kwa wavuvi wengine,” alisema Bulayi.

Mkurugenzi huyo alisema kupitia warsha hiyo wavuvi watakuja na taratibu mpya zitakazowasaidia kuwainua kiuchumi, kuvua kwa tija pamoja na kusaidia sekta hiyo kuchangia pato la uchumi wa taifa.

Alisema warsha hiyo inaonesha dhamira ya serikali kuona kwamba wavuvi wanavua kwa tija na kupiga hatua katika biashara wanazofanya.

Mvuvi, Ester Kunambi kutoka jijini Dar es Salaam akizungumza katika warsha hiyo aliiomba serikali kufungulia uvuvi wa mchana wa dagaa na samaki ili watumie vilivyo fursa katika sekta hiyo kujinua na kuondokana na umaskini.

Kunambi alisema uvuvi wa dagaa majira ya mchana ulikuwa unawasaidia sana kupata bidhaa hiyo kwa wingi pamoja na samaki,lakini baada ya kuzuia suala hilo imekuwa vigumu kwao kujiendesha ikiwamo urejeshaji wa mikopo .

Alisema serikali inapaswa kuwaangalia wavuvi wadogo ili nao waweze kusonga mbele katika uvuvi ambao utawasaidia kujiinua kiuchumi.

Ofisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo, Upendo Hamidu alisema anaamini kile ambacho kitajadiliwa kitakuja na dhana ambayo itasaidia wavuvi kupata kipato ambacho kitawasaidia kuongeza pato lao.

Chanzo: www.habarileo.co.tz