Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wataka wabeba mimba wachapwe viboko, wanaharakati wapinga

33333 Pic+mimba Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mkuranga. Baadhi ya wazee wa Kijiji cha Kiziko wilayani Mkuranga, wamependekeza wasichana wanaopata mimba shuleni bila kubakwa wachapwe viboko 12 siku 40 baada ya kujifungua.

Hata hivyo, pendekezo la wazee hao limepingwa vikali na wanaharakati wa masuala ya kijinsia wakisema, suala hilo halihitaji nguvu kupambana nalo isipokuwa kampeni za ushawishi, hekima na malezi mazuri.

Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali ukiwamo namba 2 wa 2016 ukibainisha kuwa watakaowapa wanafunzi mimba wafungwe miaka 30 jela.

Wakizungumza wakati wa kampeni ya kupambana na tatizo la mimba na ndoa za utotoni inayoendeshwa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na masuala ya kisaikolojia kwa watoto (REPPS) wilayani Mkuranga, wazee hao walisema baadhi ya wasichana wamekuwa wakisababisha kupata mimba licha ya kuwa sheria zinambana mwanamume pekee.

Mzee Hemed Mtumbo alisema adhabu ya viboko 12, itakuwa fundisho kwa wanafunzi wanaoingia kwenye masuala ya kimapenzi kwa kupenda wenyewe wakati wanajua madhara ya mimba kwenye umri mdogo.

“Ikibainika msichana alijirahisisha kwa mtoto wa kiume au alikubali mwenyewe na wala hakubakwa, apewe adhabu ya kucharazwa fimbo tu ili akawasimulie wenzake, wasijiingize kwenye vishawishi kwa kisingizio cha umaskini,” alisema.

Alisema ni kweli kwamba sheria inambana zaidi mtoto wa kiume anayebainika kumpa mimba msichana wakati wapo wasichana ambao ni sababu za mimba hizo.

“Watakuwa wanasoma wote darasa moja, msichana amepata mimba na mvulana anatakiwa kufungwa miaka 30 jela, hii sio sawa. Hata huyu wa kike acharazwe tu,” alisisitiza.

Alisema wanachopigania ni kulinda heshima na maadili ya watoto wa kike na wa kiume kila ili mmoja ajue kwamba hapaswi kuanza uhusiano wa mapenzi akiwa bado shuleni.

Bibi Mwasaburi Ally Kilungi (88), alisema wasichana wengi wa siku hizi hawana maadili na baadhi yao wamekuwa wakidharau maonyo ya wazee.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kiziko, Benjamin Mwang’ombe alisema, “Tatizo huwa linaanzia pale mtoto anapochezwa akiwa bado mdogo, huko anafundishwa kila kitu na mwishowe anaenda kufanyia kazi,” alisema.

Akizungumzia pendekezo hilo, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Eda Sanga alisema fimbo si suluhisho la mimba na ndoa za utotoni.

“Wazee wenyewe wanaweza kuzungumza na watoto wao kwa hekima wakiwaeleza madhara ya mimba za utotoni, wataelewa na kubadilika,” alisema.

Mkurugenzi Mkazi wa Repps, Edwick Mapalala alisema wameanzisha kampeni hiyo ili jamii ijadili tatizo la mimba shuleni na ndoa za utotoni.



Chanzo: mwananchi.co.tz