Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wataka jengo la Mahakama lililoachwa miaka 10 litumike

4749 COURT Wataka jengo la Mahakama lililoachwa miaka 10 litumike

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKAZI wa kata ya Ijumbi, wilayani Muleba wameomba jengo lililojengwa na mfadhili na kukabidhiwa kwa Idara ya Mahakama lianze kutumika ili kuwasogezea huduma za Mahakama karibu.

Waliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kwamba, jengo hilo lililojengwa na mfadhili, Prosper Rweyendera kwa kushirikiana na wananchi na kukabidhiwa kwa Idara ya Mahakama zaidi ya miaka 10 iliyopita bado halijaanza kutumika mpaka sasa.

“Hakuna huduma za Mahakama katika tarafa yetu ya Nshamba hali inayotulazimu kutembea zaidi ya kilometa 10 kwenda tarafa za Kashasha na Kamachumu. Watu wengi wanapoteza haki zao kwani hawana uwezo wa kuhudhuria mahakamani kutoka na urefu wa safari,” alisema mmoja wa wananchi hao, George Kahatano.

Mtendaji wa kata hiyo, Salehe Mruma alikiri kuchelewa kuanza kwa huduma za Mahakama katika jengo hilo licha ya viongozi kutembelea jengo hilo mara kwa mara.

Alisema uhaba wa watumishi ni mojawapo ya sababu zinazotolewa na Idara ya Mahakama kama changamoto kubwa ya kuchelewa kwa huduma hiyo.

“Mimi nimehamishiwa hapa hivi karibuni lakini kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, jengo hilo lilikabidhiwa miaka mingi na kupokelewa. Tumekuwa tukiwasiliana na idara husika mara kwa mara ili jengo lianze kutumika kwani ukosefu wa Mahakama ni mojawapo ya changamoto kubwa hapa,” alisema Mruma.

Alimpongeza Rweyendera kwa ushirikiano wake na wanajamii katika kuleta maendeleo ndani ya kata hiyo.

Mbali na jengo la Mahakama, Rweyendera pia amefadhili ujenzi wa kituo cha polisi, ofisi mbili za Chama Cha Mapinduzi (CCM), nyumba za watumishi wa umma wa taasisi zote za serikali, majengo matatu ya kituo cha afya pamoja na madaraja manne.

Alisema madaraja hayo yamesaidia kuimarisha mawasiliano kwani wanavijiji walikuwa wakitengana nyakati za mvua kubwa kutokana na miundombinu ya barabara kuharibika.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili limefanikiwa kupata nakala yake, Idara ya Mahakama kupitia ofisi ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ililipokea jengo hilo na kuthibitisha kwamba linafaa kwa matumizi ya shughuli za Mahakama.

Chanzo: habarileo.co.tz