Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watafiti, madaktari Ngorongoro kuchunguza kifo cha Faru Fausta

90274 Faru+pic Watafiti, madaktari Ngorongoro kuchunguza kifo cha Faru Fausta

Mon, 30 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ngorongoro. Timu ya watafiti na madaktari wa mifugo kutoka taasisi mbalimbali nchini, imetua katika Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, kwa ajili ya uchunguzi wa kina kujua sababu za kifo cha Faru Fausta (57) aliyeweka  rekodi ya kuwa faru mzee zaidi duniani.

Faru huyo, ambaye alifariki Ijumaa  Desemba 27 saa 2;17 usiku, akiwa katika banda maalumu alilokuwa amehifadhiwa katika eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro amekuwa gumzo katika vyombo vya habari duniani.

Mtafiti Mkuu mwandamizi wa Tawiri, Dk Ernest Mjingu anasema  wamefika leo Jumapili Desemba 29,2019 katika hifadhi hiyo kufanya utafiti ili kujua chanzo cha kifo cha Faru huyo, kitaalamu licha ya kuwa alikuwa na umri mkubwa sana.

“Tunaendelea utafiti  bado, tunafanya testing, tunachukua sampuri tutapeleka maabara,  lakini kubwa alikuwa ni mzee sana, tayari tumeona moyo ulikuwa umekosa nguvu ya kusukuma damu mwili,” amesema.

Amesema taarifa ya uchunguzi itatolewa baada ya wiki mbili ama tatu, ili kuweka sawa historia yake hadi kifo chake kwa ajili ya utafiti pia wa Faru maeneo mengine duniani.

Katika utafiti huo, pia wanashiriki madaktari wa wanyamapori kutoka Mamlaka ya hifadhi ya hiyo, pamoja na wataalamu wa Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Wataalamu wengine ambao walikuwa katika mchakato huo wa utafiti ni Kamishna wa uhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Dk Fredy Manongi  na Mratibu wa taifa wa uhifadhi wa faru, Filbert Ngoti.

 

Akizungumzia kifo hicho, Ngoti anasema watafiti watachukua  sampuri  na kupeleka maabara kwa utafiti zaidi  ili kujua chanzo cha kifo chake.

“Kifo chake kina punguza ongezeko la Faru kwani alikuwa jike, kwenye uhifadhi ukiondoa jike, umepunguza uzao, jike ndio dhahabu yetu, pigo kubwa sana,” anasema.

Dk Manongi anasema moja ya sababu zilizosababisha kifo cha Faru Fausta ni umri mkubwa kwa sababu amevunja  rekodi ya kuishi.

Faru Fausta ni miongoni mwa Faru ambao walikuwa na umaarufu mkubwa na mwaka juzi, matunzo yake yalitikisa bunge la jamhuri baada ya kuelezwa anatumia sh 64 milioni kwa mwezi, kwa kutokana na kununulia chakula nje ya nchi, kuwa na walinzi na kumpa mahitaji mengine muhimu.

Hata hivyo, baadaye Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ililazimika kuanzisha shamba maalum la majani aina ya lucina yenye virutubisho kwa ajili ya Faru huyo ili kupunguza gharama na kufanikiwa kwa  kiasi kikubwa.

Faru huyu alikuwa kivutio kikubwa cha watafiti duniani kote na watalii, ambao walifika Ngorongoro kumuona na kuongeza mapato ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na gawio la serikali kwa Serikali.

Chanzo: mwananchi.co.tz