Tabora. Wataalamu wa anga kutoka jijini Dar es Salaam wameanza uchunguzi wa ajali ya ndege iliyoanguka Jumamosi Agosti 3, 2019 wilayani Sikonge Mkoa wa Tabora na kusababisha vifo vya watu wawili.
Ndege hiyo yenye usajili ZU-TAF aina ya SLG4 ilikuwa ikiruka kutoka kiwanja cha ndege cha Tabora kuelekea kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Lilongwe, Malawi. Ilianguka muda mfupi baada ya kuruka.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Agosti 6, 2019 mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri amesema wataalam hao wamewasili juzi na jana wameanza uchunguzi wao kwenye eneo la ajali.
Amebainisha kuwa bado hajaonana na wataalam hao kutokana na kushiriki ufunguzi wa maonyesho ya Nanenane Kanda ya Magharibi.
Awali ilielezwa kuwa chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu ya injini, rubani alitoa taarifa katika kituo cha kuongozea ndege jijini Dar es Salaam na mara baada ya taarifa hiyo ndege hiyo ilipoteza mawasiliano na kuanguka.
Miili ya watu hao, Desmond Roy Werner (rubani) na Werner Froneman (mhudumu) lihifadhiwa katika Hospitali ya Kitete, Tabora.
Habari zinazohusiana na hii
- Ndege yaanguka Tabora, rubani na mhudumu wafariki
- Wasimulia walivyoshuhudia ndege iliyoua wawili ikianguka