Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wastaafu, watumishi Ukerewe waidai halmashauri bilioni 8/-

36073277745ff78cd883fea1ab3ada04 Wastaafu, watumishi Ukerewe waidai halmashauri bilioni 8/-

Tue, 16 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

Wastaafu na watumishi wanaoendelea na kazi wanaidai Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza Sh bilioni nane.

Fedha hizo zinatakiwa kuwasilishwa katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Ester Chaula alisema hayo jana wakati akijibu maswali madiwani kwenye baraza la madiwani.

Alisema ipo changamoto kubwa ya malipo ya kiinua mgongo kwa watumishi waliostaafu, ambao fedha za makato yao hazijawasilishwa kwenye mfuko huo.

Alikuwa akijibu swali la Diwani wa Kata ya Murutungulu, Nicolaus Munyoro aliyetaka kujua mpango uliopo wa kulipa stahiki za wastaafu ili waondoke kwenye nyumba za serikali na kutoa fursa kwa watumishi walio kazini kuzitumia.

Chaula alisema Sh bilioni nane ambayo haijawasilishwa kwenye mfuko kwa ajili ya mafao wastaafu na wale ambao wanaendelea na kazi ni kubwa, hivyo deni litalipwa kulingana na wanavyopata fedha.

Akifafanua, alisema tatizo hilo ambalo hasa linawahusu watumishi wanaolipwa kwa vyanzo vya mapato ya ndani, linatokana na upungufu wa fedha kuanzia mwaka 1990, ambapo wakati mwingine hulipa mishahara bila kuwasilisha makato yao kwenye mfuko.

Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Ilangala, Salome Marck alisema tatizo la malipo ya wastaafu ni kero kubwa kwa watumishi waliotumikia serikali kwa muda mrefu na baada ya utumishi wao wanaishi maisha magumu na wengine wanashindwa kurudi kwao.

Akijibu swali la Diwani wa Kata ya Bukindo, Grigory Kalala aliyetaka kujua lini itatengwa fedha kwa ajili ya kulipa posho ya madaraka kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwa kazi wanayofanya ya kusimamia maendeleo, Chaula alisema viongozi wanatakiwa kulipwa kutokana na asilimia 20 ya fedha za maendeleo ya kata zinazopelekwa kila mwezi.

Alisema katika mwaka wa fedha 2020/2021, Sh milioni 36.3 zimetengwa kwa ajili hiyo na mpaka sasa katika vijiji vyote 76 zimepelekwa Sh milioni tisa.

Hivyo, aliwashauri madiwani kuhakikisha viongozi hao wa vijiji na vitongoji, wanalipwa posho zao ili kuwatia moyo katika majukumu yao.

Chanzo: habarileo.co.tz