Dar es Salaam. Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy amewataka wastaafu wa taasisi hiyo kutumia vizuri fedha zao za kiinua mgongo ili kuepuka kudhalilika.
Amesema wasipokuwa na nidhamu hata fedha wanazolipwa kama kiinua mgongo zitakwisha na wataishia kudhalilika kama inavyowatokea wastaafu wengi nchini.
Mkeremy ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 5, 2019 mjini Morogoro wakati wa mafunzo ya kujiandaa na maisha baada ya kustaafu kwa watumishi 69 kati ya 78 wa TFS wanaotarajiwa kustaafu kuanzia 2019 hadi Agosti 2020.
“Mimi sijastaafu hivyo sitaweza kuwafunza kuhusu maisha baada ya kustaafu ila ninachoweza kuwaambia mimi naupenda sana ule mlio unaotoka kwenye ATM hasa ukisikika kwa muda mrefu, utasikia paraaaaaaaah nina uhakika nanyi mnapenda mlio huo.”
“Niwakumbushe kuwa na nidhamu na fedha mtakazo kwenda kupata kama kiinua mgongo licha ya wingi wake, msipokuwa na nidhamu ya fedha zitaisha na kisha kudhalilika,” anasema
Kwa upande wakem, Kamishna wa uhifadhi Profesa Dos Santos Silayo amesema wametoa mafunzo hayo kwa kuwa TFS inatambua mchango wa watumishi hao kwa usalama na uhai wa rasilimali za misitu.
Pia Soma
- Takukuru yawakamata viongozi wawili kwa rushwa ya Sh20,000
- Tango, Tucta na CCT zaitaka Sadc kuchukua hatua kinachoendelea Afrika Kusini
- VIDEO:Tanesco yatoa Sh11.5 milioni kwa mgonjwa anayepumulia mashine
“Kutokana na mchango huo tumeamua sisi kama taasisi kuwatunuku vyeti mwaka huu, vyeti hivyo vitaambatana na kishika mkono,” amesema Profesa Silayo