Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasomi Duce 'wafundwa' usawa wa jinsia

Thu, 22 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wanafunzi wa kike kwenye Chuo Kikuu kishiriki (DUCE) wametakiwa kutokuwa nyuma katika kujitokeza kugombea uongozi wa juu wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo kwa kuamini nafasi hizo zinawafaha wanaume.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni wakati wa warsha ya masuala ya jinsia Chuoni hapo iliyoandaliwa na Chuo hicho kwa ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la Woman Fund Tanzania.

Warsha hiyo imewashirikisha wanafunzi mbalimbali wa mwaka wa kwanza walioingia chuoni hapo hivi karibuni kwa lengo la kuwandaa kifkira katika usawa kabla ya kuanza masomo rasmi.

Mratibu wa warsha hiyo, Dk Ikupa Moses amesema Chuo Kikuu kishiriki cha Duce kinahitaji usawa, hivyo kilifanya warsha hiyo ili kuwaandaa wanafunzi wapya walioingia chuoni hapo hususani wa kike kuamini wako katika mazingira salama yenye usawa kwa jinsia zote.

Ofisa Misaada wa Woman Fund Tanzania, Frank Kisare amesema wameamua kushirikiana na chuo hicho ili kuimarisha klabu ya jinsia chuoni hapo  ambayo  kimejikita pia katika masuala ya usawa wa kijinsia.

"Woman Fund Tanzania moja ya kazi zetu ni kutetea na kukuza uelewa wa haki za wanawake, tunaamini mwanamke ukimjengea uwezo hatetereki, kwani uwezi kumpa mtaji bila elimu," amesema Kisare.

Amefafanua  kwamba shirika hilo linashirikiana na chuo hicho kwa kuwa, eneo hilo ni mahala huska katika kupaza sauti ya masuala ya jinsia, kwani wanaamini hata baada ya kumaliza masomo, watakuwa mabalozi wazuri wa masuala ya jinsia hata baada ya kuajiliwa.

Mgeni rasmi katika warsha huyo, Dk Neema Mogha aliyemuwakilisha mkuu wa chuo hicho, Profesa Bernadetha Killian, alisema warsha hiyo ni 'dozi' ya kuhakikisha wanafunzi hao wanaishi salama katika kipindi chote cha miaka mitatu watakayokuwa chuoni.

"Nyinyi ni wanafunzi lakini walimu, hivyo hata baada ya masomo yenu hapa Duce, tunategemea mtakapokuwa kazini mtakuwa waelimishaji wazuri wa masuala ya jinsia, bila kujali ni mwanaume au mwanamke," alisema.

Amesema wanawake wanapaswa kutoogopa na kujiweka nyuma huku akiwatolea mfano wa mkuu wa Chuo hicho, Profesa Bernadetha kuwa mwanamke ambaye katika harakati zake za masomo alipitia changamoto, lakini alikabiliana nazo na kushinda na sasa ni profesa.

"Mnapokuwa chuoni mkumbuke maagano ya mwisho na wazazi na walezi wenu, siku mnaaondoka kuja Chuoni, mkikumbuka hayo mtakuwa salama na mtakuwa msaada kwa familia hususan wanawake," amesema.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa kwenye warsha hiyo ni rushwa ya ngono vyuoni na kwenye kazi, usawa wa kijinsia na maisha salama kwa wanafunzi wa vyuo huku wanafunzi wakipewa historia ya mkuu wa chuo hicho,profesa Bernadetha alivyoanza shule akiwa hana viatu, lakini hakukata tamaa.



Chanzo: mwananchi.co.tz