Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasomewa mashitaka 460 kwa saa tano

Ceo D . Law Wasomewa mashitaka 460 kwa saa tano

Sat, 15 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetumia saa tano kwa kuwasomea mashtaka 460 wafanyakazi wawili wa Kampuni ya Usafirishaji ya Usangu Logistics, likiwamo la wizi wa Sh 428,030,000.

Wafanyakazi hao ni Katibu Muhtasi Tamal Rashid (24) na Meneja wa Kituo cha Kampuni hiyo, Salim Salim (37), wote wakazi wa Dar es Salaam.

Mashitaka hayo yalisomwa jana na jopo la mawakili watano wa serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Grace Mwanga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amri Msumi, kuanzia saa 6:00 adhuhuri hadi 11:00 jioni.

Mwanga alidai kuwa washtakiwa hao wanatuhumiwa kula njama, kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo 229 kwa mtu aliyefahamika kwa jina na Brigita Banda kwa lengo la kujipatia kiasi hicho cha fedha.

Alidai kuwa washtakiwa hao walighushi nyaraka 229 za malipo na kuonyesha kwamba ni halisi na zimetiwa saini na wakurugenzi wa kampuni hiyo, Hydar Ismail na Sadkhan Ismail, huku wakijua si kweli.

Inadaiwa kuwa washtakiwa baada ya kughushi nyaraka hizo, waliziwasilisha kwa Banda kwa ajili ya malipo ya Sh. 428,030,000 huku wakijua nyaraka hizo ni za kughushi.

Mwanga alidai kuwa washtakiwa hao ambao walikuwa waajiriwa katika kampuni hiyo, walitenda makosa hayo kati ya Desemba 23, 2021 na Novemba 6, 2022 katika eneo la Tabata Matumbi ndani ya wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.

Katika shitaka la 460, washitakiwa wanadai kuwa katika tarehe hizo zilizotajwa, wakiwa waajiriwa wa Usangu Logistics, waliiba Sh. 428,030,000 wakiwa eneo la Tabata Matumbi, Dar es Salaam.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washtakiwa walikana kuhusika na madai hayo, hivyo mahakama kuwataka kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja aweke Sh. 214,015,000.

Hakimu Msumi alisema kama mdhamini atashindwa kuweka fedha hiyo, basi atatakiwa kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo na pia hawatatakiwa kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.

Washitakiwa hao walitimiza masharti hayo ya dhamana kwa kuwasilisha mahakamani hapo hati na ripoti ambayo inaonyesha thamani ya majengo.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Neema Moshi aliomba mahakama iteue mtu wa kwenda kwenye wizara husika ili kujiridhisha uhalali wa hati hizo licha ya kwamba zina ripoti ya thamani.

Hakimu Msumi aliahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya hatua hiyo ya kujiridhisha  hati hizo na washtakiwa walirudishwa mahabusu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live