Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasiwasi watawala usajili mpya wa simu

52683 Pic+simu

Wed, 17 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) itangaza kuwa kuanzia Mei mosi watumiaji wote wa simu wanapaswa kusajiliwa kwa kutumia Vitambulisho vya Taifa, wananchi wamelalamikia ucheleweshaji wa kupata nyaraka hiyo.

TCRA imesema uamuzi wa kusajili simu kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa unalenga kudhibiti wizi na usalama wa wateja.

Lakini wananchi, ambao wamekuwa wakijazana kwenye ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho (Nida), ambayo hutoa vitambulisho hivyo wamelalamikia ufanisi wa ofisi hiyo wakisema inawachukua muda mrefu kuvipata.

Wakizungumza na Mwananchi kwenye ofisi za Nida wilayani Temeke, Dar es Salaam wananchi hao walisema wamekuwa wakipata usumbufu kutokana na kutakiwa kupeleka nyaraka tofauti, uwezo wa ofisi hizo kuhudumia watu wengi na pia kuchelewa kupata vitambulisho hivyo.

Mmoja wa wananchi hao, Salum Hamisi alisema ameanza kufuatilia juzi, lakini kila akifika ofisi hizo anaishia nje kutokana na walinzi kumueleza kuwa watu wameshajaa.

Mkazi mwingine, Mohamed Nassoro alisema ameanza kufuatilia kitambulisho tangu mwaka jana na kwamba aliahidiwa akifuate baada ya mwezi mmoja.

“Baada ya mwezi wakaniambia nikahojiwe Uwanja wa Taifa kulikuwa na ofisi zao ndogo pale, nikaenda ilikuwa Februari 18, 2018, nikaenda uhamiaji kwa ajili ya kuhojiwa nimeleta majibu ya uhamiaji,” alisema.

“Napo nimeambiwa nije baada ya kumalizika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ukiangalia ni sawa na mwezi mmoja na nusu.”

Edith Soko alisema kuwa alijiandikisha tangu mwaka 2015, lakini hadi sasa hajapata kitambulisho chake.

“Kama leo nimekwenda Kata ya Makangarawe, wakaniambia nije hapa Chang’ombe Nida. Nimekuja hapa wameniambia niende Makangarawe, nimeenda wameniambia vitambulisho vipo huku ndiyo nimerudi tena,” alisema.

“Cha kustaajabisha nimefika hapa mara mbili ndani ya siku moja na bado wamenipa namba huku wakiniambia hawawezi kunihakikishia nitakipata lini.”

Kaimu Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa TCRA, Same Mwakyanjala alisema taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo inahimiza kila mwananchi kuwa na kitambulisho cha Taifa kwani kuanzia tarehe hiyo usajili wa laini utahitaji kitambulisho hicho isipokuwa kwa mazingira maalumu ambayo hakuyataja.

Alisema kwa raia wa kigeni wanasajiliwa kwa kutumia vitambulisho vinavyowatambulisha hapa nchini.

Akizungumza na Mwananchi, mkurugenzi mkuu wa Nida, Dk Anold Kihaule alisema utaratibu wa kujiandikisha haujabadilika na kwamba vitu vinavyotakiwa kuwasilishwa kwa ajili ya mchakato huo ni vilevile.

Miongoni mwa vitu hivyo ni cheti cha kuzaliwa, barua ya mtendaji na vyeti vya elimu.

Soma zaidi: TCRA yazionya kampuni za simu

Ofisa mmoja wa kampuni ya huduma za simu nchini (jina lake limehifadhiwa), alisema huenda baadhi ya kampuni zikapungukiwa na wateja kama Nida haitakuwa na kasi ya kutoa vitambulisho.

“Kusajili laini ni dakika chache tofauti na kupata kitambulisho,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz