Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasichana wa kazi wageuka Lulu

49734 Pic+wasichana

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wasichana wa kazi za ndani maarufu ‘House Girl’ wamegeuka lulu na upatikanaji wao umekuwa mgumu ikielezwa kuwa moja ya sababu ni shule za sekondari za kata na elimu bila malipo.

Hali hiyo inawafanya waajiriwa kuwa katika wakati mgumu kuwatafuta huku wengi wao wakishindwa kumudu ujira mkubwa wanaohitaji.

Kwa sasa wasichana hao wanataka kulipwa sio chini ya Sh50,000 na hii haijumuishi chakula, malazi na matumizi mengine kama matibabu ambayo mwajiri hulazimika kumgharamia.

Mikoa ambayo imekuwa ikitoa wasichana wengi wa kazi ni Dodoma, Iringa, Tanga, Manyara, Singida na Kilimanjaro hususan maeneo ya Kibosho, Rombo, Kihurio, Ndungu na Makanya.

Miaka ya nyuma wasichana hao walikuwa wakipatikana kirahisi na kwa bei za kawaida ambazo kila mtu mwenye uhitaji alikuwa akimudu lakini sasa hali ni tofauti.

Joseph Woiso kutoka Shirika la Restless Development alisema, kwa sasa hakuna wasichana wanaohitaji kazi za ndani kwa kuwa wengi wanaohitimu darasa la saba wanaendelea na masomo.

Alisema hiyo ni habari njema kwa kuwa kwa sasa jamii ina uelewa na wazazi wengi wanatambua haki za watoto ikiwamo kupatiwa elimu.

Woiso alisema kwa sasa elimu imepewa kipaumbele na watoto wengi wanafaulu tofauti na zamani ambapo ilikuwa mwanafunzi anachaguliwa kujiunga na sekodari na si kuangalia kama alifeli. “Mzazi alikuwa anakosa namna ya kufanya mtoto akifeli, anaona bora ampelekea mjini akafanye kazi. Kwa sasa wanafunzi wengi wanafaulu kwenda sekondari,” alisema Woiso.

Hata kwa wale wanaokwenda kufanya kazi za ndani, Woiso alisema wengi wanajua haki zao ndio maana hutoa masharti.

Mwanaharakati wa masuala ya wanawake na jamii, Queen Issack alisema, Serikali ya Awamu ya Tano haina mzaha na wazazi wanaogopa kuchukuliwa hatua za kisheria mtoto asipohudhuria masomo.

Alisema, “zama zinabadilika, kwa sasa kupata wasichana wa kazi labda usubiri wamalize kidato cha nne na mtu aliyemaliza kidato cha nne asipofanikiwa kuendelea anaona bora aende akaolewe kuliko kufanya kazi hiyo.”

Queen ambaye ni mwandishi wa habari wa gazeti la Daily News mkoani hapa, aliongeza kuwa sera ya elimu bila malipo imewafanya wazazi wengi kuacha ulimbukeni na kuwapeleka watoto wao shule.

Waajiri waeleza ugumu

Agness Mushi ambaye ameajiriwa katika sekta isiyo rasmi, alisema ni muda mrefu amekuwa akihangaika kupata dada wa kazi bila mafanikio.

Alisema dada ambaye alikuwa akiishi naye aliondoka kwa kurubuniwa na mtu mwingine hajapata mwingine hivyo kumlazimu mtoto wake ambaye yuko chekechea kushinda shule.

Adha ya dada wa kazi pia inamkabili Shamsa Ally ambaye alisema, “Nilipata safari kwenda nyumbani nikaona nimpe nafasi binti yangu wa kazi naye aende nyumbani kwao Dodoma kusalimia. Niliporudi aligoma baada ya wazazi kumtafutia mchumba.”

Alisema baadhi ya watu wanafanya utapeli kwa kuwa amewahi kutuma nauli mara kadhaa kwa ajili ya kuletewa lakini fedha zimeliwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz