Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasichana Korogwe wanavyokwepa kurudi shule baada ya kujifungua

Mimba Mashuleniiii Wasichana Korogwe wanavyokwepa kurudi shule baada ya kujifungua

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ilinichukua kati ya saa mbili na dakika 30 hadi tatu nikitumia usafiri wa pikipiki (bodaboda) hadi kufika Kijiji cha Mashewa kilichoko Kata ya Mashewa katika halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.

Ilikuwa ni safari kupitia barabara ya vumbi ambayo ilinigharimu Sh50, 000 kwa maana ya kwenda na kurudi.

Lengo la safari yangu lilikuwa ni kufuatilia utekelezaji wa mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali, wakiwamo wale waliopata ujauzito. Waraka huo wa Februari 2022, ni mwongozo huu unaotoa maelekezo yatakayowezesha urejeshwaji wa wanafunzi waliokatiza masomo ili waweze kukamilisha mzunguko wa masomo yao katika mfumo rasmi. Wanafunzi hao ni pamoja na wale waliopata ujauzito masomoni.

Ni uamuzi ulioshangiliwa na wapigania haki hasa za watoto wa kike ambao kwa muda mrefu walikuwa wakiusubiri kwa shauku kubwa. Waliamini kuwa utaratibu wa awali wa kuwafukuza waliopata ujauzito, ulikuwa kikwazo kikubwa kwa mtoto wa kike.

Hali ilivyo Korogwe

Baada ya safari ndefu ya kuifuata sekondari hiyo ya Mashewa inayotegemewa na vijiji tisa, ndipo ninapobaini kwamba hakika ‘Penye miti hakuna wajenzi’ kwani si wasichana wenyewe wala jamii kwa ujumla katika Halmashauri ya Korigwe wanaoichangamkia fursa hiyo ya kurejea shule iliyotolewa na serikali.

Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Suleiman Hamad anasema ujauzito siyo changamoto inayowasumbua kwani ni aghalabu kutokea matukio ya aina hiyo na kwamba mwaka jana ni mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu aliyebainika kuwa na ujauzito, lakini hivyo binti huyo aliondoka nyumbani kwao.

“Yule binti alivyobainika kuwa ni mjamzito tukamruhusu akae nyumbani na arudi shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua, ila taarifa nilizonazo hayupo. Huku mwamko wa elimu ni mdogo kuna uwezekano kabisa familia imeshiriki katika kumuondoa au yeye mwenyewe amejiona kuwa tayari ameshakuwa mtu mzima hawezi kusoma tena,”,anasema Hamad.”.

Mazingira kama hayo yapo pia katika sekondari ya Chekelei ambako Mkuu wa shule hiyo, Jorwa Musiangi anakiri kwamba mwanafunzi aliyepata ujauzito shuleni hapo alikataa kurejea shuleni na kuondoka kijijini.

“Mwaka 2021 tulikuwa na kesi ya ujauzito ya mwanafunzi wa kidato cha pili, alikuwa miongoni mwa wanaotakiwa kurudia darasa hilo baada ya kufeli mtihani wa taifa. Alirudi shuleni lakini baadaye ikagundulika kuwa ni mjamzito tukamwambia apumzike nyumbani hadi pale atakapoji fungua arejee shuleni.

“Tofauti na matarajio yule mtoto ndiyo ikawa amepotea moja kwa moja, muda ulipopita tuliendelea kumfuatilia kwa wazazi wake na hatimaye tukatoa taarifa Serikali yaiKijiji na alikataa kabisa kurudi shule na akaondoka tukasikia kwamba amekwenda Zanzibar,” anasema Musiangi.

Katika halmashauri ya wilaya ya Korogwe, takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2021 wanafunzi wa sekondari 10 walipata ujauzito, mwaka 2022 wanafunzi 10 na mwaka 2023 tayari wanafunzi 11 wamepata ujauzito wakiwa shuleni.

Licha ya takwimu hizo, hakuna msichana yeyote aliyerejea shuleni baada ya kujifungua licha ya Serikali kutoa fursa hiyo huku uchunguzi wa Mwananchi ukibaini kuwa pindi mtoto wa kike anapobainika kuwa na ujauzito anahamishwa kijijini kukwepa mkono wa sheria.

Mwenendo wa wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shuleni katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kutokata kurejea kuendelea na masomo, inaweza kuwa tofauti na ilivyo katika halmashauri nyingine ambako wasichana kama hao wanatamani kurejea na kuendelea na masomo.

Utafiti uliofanywa taasisi ya Msichana Initiative katika wilaya za Kongwa mkoani Dodoma na Nzega, mkoani Tabora .

Kuhusu utekelezaji wa mwongozo wa kurudi shule kwa wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu ya ujauzito, ulibaini kuwa wasichana wanane kati ya 10 waliopata ujauzito sawa na asilimia 85 wanatamani kurejea shule kuendelea na masomo.

Kwa mujibu wa utafiti huuo, asilimia 15 ya mabinti hao iliyobaki wanahitaji kuwekewa mazingira wezeshi kwao na kwa watoto wao ili waweze kusoma bila kukutana na vikwazo ikiwemo msongo wa mawazo.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Korogwe, Halfan Magani anathibitisha kutokuwepo msichana yoyote aliyerejea shuleni baada ya kujifungua kama ambavyo mwongozo unaelekeza.

“Tunafahamu kuhusu mwongozo na sio tu ngazi ya halmashauri umeshushwa kwa maofisa elimu kata, walimu wakuu na hata viongozi wa vijiji kote huko tumeweka nguvu ya pamoja kusimamia suala hili lakini ninachoweza kusema kwa upande wa mabinti waliopata ujauzito hakuna aliyerejea shuleni.

“Kama ambavyo mwongozo umeelekeza upande wa Serikali tunatimiza wajibu wetu, wakuu wa shule wameweka mazingira wezeshi, walimu wako tayari kuwapokea hao watoto lakini tunaiona changamoto kwenye jamii mwamko wa elimu ni mdogo,” anasema Magani.

Wanaokutwa na ujauzito kuhama Mwananchi limebaini kuwa, licha ya kufunguliwa milango ya kurejea shuleni pale wananfunzi wanapojikuta kwenye hali ya ujauzito huamua kuhitimisha safari yao ya elimu.

Walimu waliozungumzia hali hii, wanaelekeza lawama kwa zao kwa wazazi wakisema wanachangia kwa kiasi kikubwa katika kufanya watoto wasirudi shuleni kwa kile wanachoona kwamba mtu akishabeba ujauzito tayari ni mtu mzima hivyo hawezi kusoma.

Juma Shekifu ambaye ni mkazi wa kijiji cha Madumu kata ya Chekelei anasema baadhi ya wazazi huwahamisha watoto wao kwa kukwepa aibu na maumivu ya kunyooshewa vidole kuwa mtoto wake ni mhuni.

“Mimi pia ni mzazi iko hivi huku kwetu suala la elimu ndiyo kama hivyo unaona si jambo ambalo linapewa uzito na watu wengi, hivyo wazazi wachache wanajitoa kupeleka watoto wao sekondari na tunafahamu kuna gharama za kufanya hivyo.

“Sasa mtu aingie gharama halafu mtoto mwenyewe aishie kupata ujauzito, kama una moyo mdogo unaweza kumpiga hadi huo ujauzito wenyewe utoke ili kuepusha kesi ndiyo unaweza kumuondoa asiwepo kwenye upeo wa macho yako,”anasema Shekifu.

Anasema mara nyingi mabinti wanaopata ujauzito hupelekwa kwa ndugu na jamaa wa vijiji au mikoa jirani hadi pale atakapojifungua na kama atapata cha kufanya huko aliko ni mara chache kurejea nyumbani.

Hilo linaelezwa pia na Mariam Shelukindo mkazi wa kitongoji cha Kwetonga kilichopo kata ya Mashewa, ambaye anasema mara nyingi kinamama wanalazimika kutafuta namna ya kuwahamisha mabinti zao wakipata ujauzito kwa kuwa lawama huangushiwa upande wao.

“Mtoto akiwa yuko vizuri ni wa familia ila akiwa na changamoto ni mzigo wa mama yake, hili hutokea zaidi kwa hawa mabinti zetu. Ni kweli Serikali imetoa fursa hiyo ya kurudi shule lakini sio rahisi kama wanavyofikiria.

“Kwanza anapopata ujauzito binti hata ndoa ya wazazi wake inakuwa shakani, baba atamsumbua mama kana kwamba alihusika katika kupatikana kwa hiyo mimba na ndiyo maana wengine wanaona bora amuhamishe ili upepo mbaya upite kwanza,”anasema. Anasema katika kipindi cha kusubiri upepo mbaya upite binti anaweza kujifungua na kupata shughuli ya kufanya hivyo suala la kurudi shule linaweza lisiwe tena kwenye mawazo yake.

“Wote tunafahamu uchungu wa mwana aujuae mzazi, ukishakuwa mama unatamani muda wote uwepo kuhakikisha mtoto wake yuko salama na utafanya kila linalowezekana kuhakikisha anapata mahitaji yake ya msingi, ndiyo maana binti anaona ni heri afanye shughuli yoyote ya kumuingizia kipato hata kama ni kulima kwa kibarua,”anasema.

Utafiti uliofanywa taasisi ya Msichana Initiative katika wilaya za Kongwa na Nzega, kuhusu utekelezaji wa mwongozo wa kurudi shule kwa wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu ya ujauzito, ulibaini kuwa wasichana wanane kati ya 10 waliopata ujauzito sawa na asilimia 85 wanatamani kurejea shule kuendelea na masomo.

Kwa mujibu wa utafiti huuo, asilimia 15 ya mabinti hao iliyobaki wanahitaji kuwekewa mazingira wezeshi kwao na kwa watoto wao ili waweze kusoma bila kukutana na vikwazo ikiwemo msongo wa mawazo.

Hilo linawafanya wengi wachague kutafuta maarifa ya nje ya mfumo rasmi wa elimu kwa kile wanachoona kurudi shuleni kutawapotezea muda na badala yake ni heri wapate mafunzo yatakayowawezesha kujiajiri ndani ya muda mfupi.

Mfano wa hilo umeonekana katika wilaya ya Kongwa ambapo wasichana 15 waliohojiwa wameonyesha wako tayari kurudi shule ingawa asilimia 50 kati yao wanahitaji zaidi kurejea katika mfumo wa elimu usio rasmi ikiwemo mafunzo ya ufundi au madarasa ya ujasiriamali yatakayiwasaidia kujifunza jinsi ya kutengeza fedha ili wawasaidie watoto wao. Wilayani Nzega utafiti umeonyesha kuwa kwa kiasi fulani kuna mazingira wezeshi kwa wasichana wanaorejea shuleni ingawa bado kuna changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi.

Baadhi ya wasichana waliohojiwa kwenye utafiti huo wametaja kukosekana kwa mabweni kwa wanafunzi wanaoishi mbali na shule, kukosekana kwa chakula, kukosekana kwa walimu wa saikolojia ambao wanaweza kuwasaidia kuwajenga kisaikolojia baada ya kurejea shule ni miongoni mwa vikwazo.

Mratibu wa vilabu ya jinsia shuleni wilaya ya Korogwe, Mariam Kawambwa anasema jitihada kubwa inafanyika katika kusimamia utekelezaji wa mwongozo wa wanafunzi waliokatisha masomo kurejea shuleni ila changamoto ipo kwa jamii na watoto wenyewe.

“Wazazi wa huku wanapelekeshwa na watoto wao, mfano hivi karibuni kuna mtoto wa darasa la sita aliamua kuacha shule bila sababu. Tulimfuatilia mzazi wake akasema hana cha kumfanya anahofia mtoto asije kujiua,’’ anaeleza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live