Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasichana 48 washindwa kurudi shule wilayani Bahi

229e5d7226d740cf7e783e0e91573c57 Wasichana 48 washindwa kurudi shule wilayani Bahi

Tue, 6 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAKWIMU kutoka shule sita za sekondari zilizopo Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, zinaonesha wasichana 48 hawakurudi tena shule kuendelea na masomo baada ya ugonjwa wa Covid-19 na mafuriko.

Imeelezwa kuwa kati yao, 17 walithitishwa kupata mimba za utotoni. Hayo yalibainika hivi karibuni wakati wa mkutano wa mradi wa kujenga uelewa juu ya unyanyasaji wa kijinsia wakati wa majanga Covid- 19 na mafuriko, kwa lengo la kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya vitendo vya unyanyasaji.

Mradi huo unatekelezwa na Marafiki wa Elimu Dodoma kwa Ufadhili wa Mfuko wa Ruzuku ya Wanawake Tanzania (WTF).

Wanafunzi hao wal iopata ujauzito ni wastani wa wasichana wanane kwa kila shule ya sekondari.

Wanafunzi hao hawajarudi tena kuendelea na masomo na kati yao wasichana watatu kwa kila shule walipata mimba za utotoni. Kulingana na taarifa hizo zilizotolewa kwenye mkutano huo, shule hizo sita za sekondari za wilaya ya Bahi ni Chipanga, Kigwe, Bahi, Mpamantwa na Ibihwa.

Imebainika kuwa katika Shule ya Sekondari ya Kigwe, wasichana sita waligundulika kuwa na ujauzito.

Pia jumla ya wanafunzi 10 hawakurudi shuleni, wakiwemo wasichana sita na wavulana wanne na kufanya idadi ya wanafunzi 16 waliokatisha masomo kipindi cha Covid-19.

Kwa Shule ya Sekondari Bahi kulikuwa na mimba mbili na wanafunzi ambao hawakurudi shuleni ni 42, wakiwemo wasichana 23 na wavulana 19.

Katika Shule ya Sekondari Chipanga wasichana wanne walipata ujauzito na wavulana watatu, hawajaripoti shuleni tangu shule zifunguliwe. Katika Shule ya Sekondari Mpamantwa, wasichana watatu waligundulika na ujauzito na ambao hawajaripoti ni 13, wavulana tisa na wasichana wanne.

Kwa Shule ya Sekondari ya Ibihwa, mwanafunzi mmoja aligundulika kuwa mjamzito na wanafunzi wote walirudi shuleni baada ya likizo ya Covid-19.

Pia kuna taarifa kuwa wasichana wawili wa Ibihwa sekondari walitoroshwa kwenda Dodoma kufanya kazi za ndani, lakini jitihada zilifanyika na wamerejea shuleni.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mratibu wa Programu wa MED, Luhaga Makunja alihoji kwa nini wastani wa wasichana wanane kwa kila shule ya sekondari wilaya ya Bahi hawajarudi tena kuendelea na masomo baada ya Covid-19 na mafuriko, lakini serikali na jamii hawajachukua hatua za kuwalinda.

Alisema kwa yeyote anayejua kwamba kuna msichana au mwanamke anayeonewa au kutendewa vibaya, kuwa na mahusiano ya mapenzi chini ya miaka 18, ubakaji, ndoa za utotoni, mimba za utotoni, kipigo kilichopitiliza, ndoa za kulazimishwa, ajira za utotoni, rushwa ya ngono na vitisho, hana budi kutoa taarifa.

Makunja alisema taarifa hizo zitolewe kwenye ofisi za ustawi wa jamii, Polisi, dawati la jinsia na watoto, ofisi za serikali za mtaa, kamati ya ulinzi na usalama wa mtoto na wanawake dhidi ya unyanyasaji, taasisi na mashirika ya kijamii kwa kupiga namba 116 ambayo huduma hiyo hutolewa bila tozo.

Kiongozi wa Asasi ya Bangonet, Nicholos Kosey alitaka jamii kuhakikisha kuwa wasichana wanalindwa na hawashiriki katika shughuli hatarishi.

Chanzo: habarileo.co.tz