Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasafiri Moshi wahofia kupoteza ajira kwa kukosa usafiri

34707 Usafiri+pic Tanzania Web Photo

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wasafiri walioshindwa kusafiri leo Alhamisi katika stendi ya mabasi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wanahofia kupoteza ajira zao kutokana na adha ya usafiri.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kituoni hapo leo Januari 03, 2019, wameiomba Serikali iongeze nguvu katika stendi hiyo kwani kushindwa kusafiri kutaleta madhara makubwa kwao.

Johnson Mmari amesema yapo madhara  yatakayojitokeza kwa baadhi ya wasafiri kutokana na wengi kulazimika kurudi tena majumbani.

"Kwa mfano mimi nimetokea Arusha nimetumia gharama kubwa kufika hapa stendi halafu ndio hivyo naambiwa usafiri hakuna. Hapa nilipo sijui nielekee wapi maana hawa wakata tiketi wananiambia hadi tarehe 10 ndio kutakuwa na nafasi," amesema Mmari.

"Wengine tunawahi kazini, sasa kama hakuna usafiri hapa ni tatizo kubwa mabosi wetu hawatatuelewa kwa hii hali.”

Amesema kuwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) hawakujipanga kwa sababu wangejipanga hali ingekuwa nzuri.

“Nitakaa hapa stendi mpaka kieleweke nikishindwa kupata usafiri leo basi liwalo na liwe, itabidi nilale kama wenzetu jana," amesema Mmari.

Agness Tesha ambaye pia ni mmoja wa wasafiri wanaokwenda mkoani Morogoro ameitupia lawama Sumatra kwa kushindwa kudhibiti upandishwaji wa nauli kiholela jambo ambalo linawaumiza.

"Hii hali kwa hapa stendi imekuwa mbaya sana, Sumatra sijui wanafanya nini mtu unaambiwa nauli Sh50,000 unaitoa wapi na hii hali ilivyo kwa sasa, huku ni kuumizana bila sababu, wengine tunawahi makazini,” amesema.

“Tutaenda wapi tukifukuzwa kazi kwa kuchelewa? Hili jambo linahitaji ufumbuzi maana hapa niko na watoto watatu na wanatakiwa kuripoti shule Jumatatu, sasa naambiwa nirudi nao kijijini tena, huu ni mtihani.”

Kwa upande wake, Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Kilimanjaro, Johns Makwale amewataka wananchi kuacha tabia ya kuitupia lawama Sumatra na badala yake wafuate maelekezo yanayotolewa na mamlaka hiyo.

"Tumeshatoa matangazo ya kutosha kwamba abiria wakate tiketi mapema ili kuondokana na usumbufu hapa stendi wa kupandishiwa nauli kiholela, lakini tunachunguza wale wote watakaobainika wanatoza nauli kubwa  tutawakamata,” amesema Makwale.



Chanzo: mwananchi.co.tz