Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasafiri Moshi – Dar wakosa usafiri, warejea majumbani

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Janeth Joseph, Mwananchi

[email protected]

 

Moshi. Mamia ya wasafiri wameshindwa kusafiri leo Alhamisi Januari 3, 2019 kutoka Moshi mkoani Kilimanjaro kuelekea mikoa mbalimbali nchini Tanzania kutokana na uhaba wa mabasi.

 

Hali hiyo inatokana na ongezeko la wasafiri katika kituo cha mabasi Moshi kutokana na abiria waliofika mkoani humo kwa ajili ya mapumziko ya mwisho wa mwaka kuanza kurejea katika maeneo yao ya kazi na makazi.

 

Leo asubuhi Mwananchi Digital imeshuhudia wananchi wakihaha kusaka usafiri na wengi wakirejea majumbani mwao kutokana na kukosa usafiri, pia nauli kuwa kubwa zaidi.

Joseph Kiluwa, mmoja wa wasafiri anayeelekea Dar es Salaam amesema ameshindwa  kusafiri kutokana na kukosa basi na nauli kuwa juu.

 

"Niko hapa stendi tangu saa 12:30 asubuhi magari hakuna na yaliyopo yote yamejaa. Nauli nazo hazishikiki. Sisi wakulima hatumudu hizi gharama, tunaomba Serikali itupie macho katika stendi hii maana wengine ni wagonjwa," amesema.

 

Amesema, "Cha kushangaza hawa wakata tiketi wakitufuata wanatuambia nauli ni Sh40,000 na Sh50,000 wakishasema hivyo hawageuki, halafu wanatuambia tutunze siri tusiseme."

 

Samweli Lazaro amesema tangu afike stendi saa 12:30 asubuhi  hakuna mabasi na yaliyopo yamejaa hata yale magari madogo hakuna.

 

"Natakiwa niripoti  kazini kesho, nisiposafiri leo bosi wangu hatanielewa. Mtu unaweza ukafukuzwa kazi kwa kukosa siku moja tu, tunaomba serikali iangalie hili jambo vizuri maana wengine tunahofia kupoteza kazi kutokana na shida ya usafiri," amesema Lazaro.



Chanzo: mwananchi.co.tz