Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waraka wa Askofu Shoo

32835 Pic+waraka Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo amesema changamoto ya umaskini nchini imesababisha manung’uniko na kukosa matumaini.

Hayo yamo katika waraka maalumu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya utakaosomwa katika dayosisi zote 26 za KKKT yenye zaidi ya waumini milioni 6.5 nchini.

Katika waraka huo, Askofu Shoo amesema jamii imeshuhudia jinsi ambavyo wanawake, watoto, vijana na jamii ya Watanzania kwa ujumla, inavyopitia katika changamoto mbalimbali.

“Kwa mfano vipo vitendo vya kikatili kama vile ubakaji, ukeketaji, ndoa za utotoni na ukatili wa kila aina,” alisema Askofu Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT. “Zipo changamoto mbalimbali zinazotokana na umaskini zinazosababisha watu kuwa na manung’uniko na kukosa matumaini. Ujumbe wa Krismasi na Mwaka Mpya utukumbushe sote kutokata tamaa.”

Askofu ametumia salamu hizo kuwataka washarika na viongozi katika ngazi zote za kanisa kuongeza bidii na maarifa katika kuwahudumia watu wote kwa moyo wa upendo na uaminifu wakati wote.

“Watu waliokata tamaa katika maisha waone ya kwamba wana matumaini mapya katika kristo. Tusiache kuwakumbuka wote wenye huzuni, wapweke,wanaoteseka, wanaoteswa na kutengwa na familia zao,” alisema.

Askofu Shoo alisema ujumbe wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni habari njema ya furaha kwa watu wote maana mabadiliko ya kweli yataonekana kwa yeyote atakayempokea Yesu Kristo katika maisha yake.

“Matokeo ya furaha hii ni amani, haki, upendo na kuthamini heshima ya utu kwa kila mmoja wetu katika jamii yetu huku tukiendelea kutunza tunu za kanisa na za nchi yetu,” alisema.

“Tunapofurahia kuupokea mwaka mpya wa 2019, namsihi kila mmoja wetu afanye maamuzi binafsi ya kujitoa zaidi kwa Mungu katika ufuasi na utumishi kwa nafasi zetu kwenye familia, jamii, kanisa na taifa.”

Salamu za Askofu Shoo zimekuja wakati waraka wa Baraza la Maaskofu wa kanisa hilo uliotolewa Aprili, 2018 ukiwa bado ukigonga vichwa vya baadhi ya viongozi, wanazuoni na wananchi.

Waraka huo wa mwaka jana, uliotiwa saini na maaskofu 26, ulielezea kuminywa kwa demokrasia, kulegalega kwa utawala wa sheria, utekaji na mauaji ya raia wema, uhuru wa mahakama na kushuka kwa elimu.

Mwaka huu, maadhimisho ya Krismasi kitaifa yatafanyika katika Jimbo Kuu la Katoliki Mwanza, yakitanguliwa na mkesha wa Krismasi utakaofanyika katika Kanisa Kuu la Epifania Bugando, Mwanza.



Chanzo: mwananchi.co.tz