Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapimbwe walivyojipamba na mila zao

Fc5874568e2a1fc9bd0b07ea72a828c9 Wapimbwe walivyojipamba na mila zao

Fri, 21 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Katika sehemu ya kwanza ya makala haya kuhusu kabila la Wapimbwe tuliona kuhusu asili yao, utawala, utamaduni na shughuli zao za kujiingizia kipato. Wapimbwe ni kabila dogo katika Mkoa wa Katavi na wanajulikana kwa kiasi kidogo sana nje ya eneo lao. Kabila hili lina lugha ya pekee na utamaduni uliotokana na misingi ya uvuvi na uwindaji. Fuatana nami katika sehemu hii ya pili kuyajua mengi yanayowahusu…

Kuzaa na kulea

Wanawake wajawazito walizalishwa na wakunga (malombwe au nakambusa) na kisha walichanjwa na kupakwa unga unaotokana na mizizi na majani ya aina mbalimbali.

Kama uzazi haukuendelea vizuri, ushauri ulitafutwa kutoka kwa wabashiri (mfumu) kutafuta sababu. Iwapo mwanamke analia kutokana na maumivu alilaumiwa na mama yake na mama mkwe wake.

Kuzaliwa kwa mapacha (amapasa) ilichukuliwa kuwa sababu ya kupata woga (wa kuwepo miungu ya uhasama) na baraka kubwa. Vilevile, jamii ilipiga kelele za aibu au kumsifu mama kwa kuzaa mapacha.

Baadhi ya hadithi zinaeleza kuwa vichwa vya wazazi vilinyolewa kwa kutumia pombe maalumu (inzubhi ya mapasa) kabla ya kupakwa mafuta na unga. Wakunga baadaye waliandaa uji maalumu (ilombo) ambao ulinywewa na familia yote kuwakinga na balaa hilo.

Mwishoni mwa kila mwezi sala ya baraka ilifanyika kwa mapacha hao (ukusasa lwanga).

Sherehe na ndoa

Wasichana walianza kufikiri kuhusu ndoa katika umri wa miaka 12, wavulana kati ya miaka 16 na 20, na walipowabainisha wachumba walitumia mshenga (kikwantemo).

Kuoa wake wengi iliwezekana kwa machifu tu, na watu wachache katika jamii. Uhusiano baina ya mashemeji ulikuwa rasmi, heshima ilikuwa inatunzwa. Wake na waume katika asili ya Mpimbwe hawakuwa wakila pamoja, wala hawakuzungumza pamoja hadharani.

Wakati mwanaume anapombainisha mke, humtuma mshenga kwa wazazi wa msichana, ambao atawatembelea asubuhi mapema na kusema “Mtu fulani amenituma kuomba maji ya kunywa kwenu.” Hii ni kusema kuwa kulikuwa na mwanaume alitaka kumwoa binti yao.

Iwapo kama hakukuwa na kipingamizi, mahari zilipangwa na baadaye jembe (inkoma lwiye) lilitolewa kama zawadi ya kwanza, ikiwa na maana “kubisha mara moja mlangoni.”

Katika mkesha wa kuolewa, bibi harusi alitoroka nyumbani. Kisha tambiko linaloitwa ukumzovya lilifanyika ambapo alipakwa majivu na matope.

Baadaye, mmoja wa mashemeji zake au mwenye uhusiano mwingine alimbeba mgongoni kutembelea kibanda cha baba yake mkubwa. Hii ilikuwa ishara ya kumuaga msichana kabla hajaiacha familia yake na kuungana na familia nyingine.

Wakati sherehe zinapokaribia kuanza, watu walienda kulima huku wakipiga vigelegele. Hili lilifanywa na shangazi wa bibi harusi (dada wa baba) kwa kugonganisha shoka na jembe, na kutoa sauti.

Kisha walicheza ngoma, na bibi harusi alipakwa chaki nyeupe (intakaso). Saa tisa kamili alfajiri shangazi alichemsha maji ya kumwogesha bibi harusi. Kisha uji wa mtama ulipikwa kwenye kibanda cha bibi harusi na bwana harusi aliruhusiwa kuingia ndani.

Katika tambiko lililoitwa akasondya, bwana harusi alimmiminia bibi harusi uji mdomoni na bibi harusi aliutema kabla ya bibi harusi kurudia mchakato kama huo kwa bwana harusi. Kisha wageni walianza kula na kucheza wakati bibi harusi na bwana harusi wakijipamba.

Bibi harusi alivaa nguo inayoitwa ‘amandingi’ kuanzia kiunoni hadi miguuni, mkufu wa shanga kuzunguka kiuno chake na mikufu miwili inayokatisha kuanzia juu kati ya matiti yake. Mwili wake wote pia ulipakwa mafuta. Nywele zake zilisukwa vizuri na kupambwa kwa majani ya asili.

Bwana harusi na mpambe wake (icinsindi) walirudi kwenye kibanda cha bwana harusi, walijipaka mafuta na kujipamba kwa mikufu.

Bwana na bibi harusi wote walivaa impazi (gamba la chaza mkubwa wa baharini) vichwani mwao na chomeka (unyoya wa ndege wa rangi mbalimbali unaoitwa inkulukulu) kwenye nywele zao.

Bwana harusi pia alibeba upinde na mshale (ubhuta), kwa ajili ya kuwazuia watu wanaoweza ‘kumchumbia’ mke wake au kujilinda.

Bibi harusi alipokuwa tayari, baba yake alimruhusu kwenda nje na kukutana na mume wake ambaye alimsubiri kwenye mlango wa kibanda, akiwa amemwegemea mfanyakazi aliyeitwa ‘intuba lya lubazi’.

Kisha baba wa bibi harusi wakati mwingine alimwimbia mke wake, akimkumbusha kutoka nje ya nyumba na kutoa maneno ya mwisho ya ushauri kwa binti yao kwa sababu mahari yameshapokelewa.

Bibi harusi alisindikizwa na kikundi cha wanawake ambao walijitambulisha kwa bwana harusi na kumhadharisha awaheshimu. Wakati haya yakitokea, ngoma ijulikanayo kama ‘itchitumba’ ilipigwa na nyimbo maalumu ziliimbwa.

Baba wa bibi harusi baadaye alitumbukiza vidole vyake viwili vya shahada pamoja kwenye chungu cha mafuta kutoka kwenye kibanda cha bibi harusi na kumpaka bibi harusi miguuni, nyuma ya mikono yake, koo lake na nyuma ya shingo yake.

Alirudia mchakato huu kwa bwana harusi kabla ya kuchukua mafuta kutoka kwenye kibanda cha bwana harusi na kufanya kazi hizo za kuwapaka mafuta wote wawili.

Baadaye, udongo kutoka kwenye kibanda cha bibi harusi ulitumika kuwapaka maharusi hao kwa njia ileile. Kisha zamu ilihamia kwa baba wa bwana harusi ambaye pia aliwapaka maharusi mafuta na kumwelekeza kijana wake kuhusu wajibu wake kama mume.

Sherehe ilipoisha, bibi harusi aliketi kwenye miguu ya shangazi yake ambaye kimila aliketi kwenye kigoda (kiti kidogo cha miguu mitatu).

Kisha bwana harusi na mpambe wake walichomoa baadhi ya majani kutoka kwenye nyumba ya baba mkwe wake mpya kuashiria kuwa sasa wameoana na binti yake na anaondoka kwenye nyumba ya familia.

Baadaye jioni hiyo, saa mbili baada ya jua kutua, dada wa bwana harusi walienda kumchukua bibi harusi na kumpeleka kwa bwana harusi. Sasa ilikuwa wakati wa tambiko kufanyika lililohusisha fedha maalumu (si mahari) zilizotolewa kwa bibi harusi kuonesha kuwa sasa aliwajibika kupikia familia.

Hadithi za zamani zinaonesha kuwa ilikuwa kazi ya shangazi wa bibi harusi kukusanya kivi na bibi harusi angekataa kuingia kwenye nyumba ya bwana harusi hadi bwana harusi atoe kiasi kinachofaa.

Shangazi pia alichukua nafasi muhimu katika kuonesha kama bibi harusi ni bikira au la, na kama habari zilikuwa njema, shangazi alipiga vigelegele. Kisha mama wa bibi harusi alipewa zawadi na mume wake kama ishara ya kuwa alikuwa mzalishaji wa ‘binti kisura’.

Kama hakuwa bikira, mama wa bibi harusi alilaumiwa na inasemekana kuwa wakati mwingine alipigwa faini na wanawake wengine. Kupoteza bikira mapema kulileta aibu kubwa kwa familia ya bibi harusi, na nyimbo ziliimbwa mara kwa mara kuwahusu.

Kifo

Mtu mzima alipokufa maji ya moto yalimiminwa kwenye kichwa cha mwili, na macho na mdomo wake vilifungwa.

Wapimbwe walizika maiti katika makaburi ya mviringo yasiyo na alama, ingawa wakati mwingine mti ulipandwa kama alama. Makaburi haya yalikuwa madogo, hivyo ilikuwa muhimu kwa miguu ya maiti kuvunjwa ili aweze kuketi sawasawa ndani ya kaburi.

Kimila, maiti ilisafishwa na wazee kwa kufunikwa na mashuka na kuzikwa. Kila mmoja aliyehudhuria mazishi alimwaga udongo kwenye kaburi, kumzuia marehemu asirudi kama mizimu.

Baada ya mazishi, wanakijiji waliomboleza kwa wanaoishi mbali kuhudhuria siku ya mwisho ya mazishi ambayo iliadhimishwa kwa kuosha mikono; wale walioshindwa kuhudhuria mazishi vinginevyo walistahili kushutumiwa kwa kutowajibika na kifo, kwa kutumia uchawi.

Siku mbili kabla ya kufanyika sherehe ya uoshaji mikono, wanaume walialikwa kwenda msituni kuwinda katika tambiko linalojulikana kama ‘ukusumba chizimu’.

Iwapo wanaume watarudi na mnyama mmoja au zaidi, kifo kiliamuliwa kuwa cha kawaida, lakini kama hakuna mnyama atakayeuawa basi hii ilifikiriwa kuwa dalili mbaya.

Iwapo marehemu alifikiriwa kulogwa, basi ndugu wa karibu zaidi wakati mwingine walizamishwa kwenye maji, ikidhaniwa wanaondoa pepo mbaya.

Mtu asiyekuwa na watoto (mwanaume au mwanamke) alizikwa na mkaa (kisunsulo) kati ya miguu yao au mgongoni mwao. Baadaye, wakati mtu mwenye ukoma au kigugumizi alipokufa, alipelekwa ufukweni mwa mto na kutupwa kichakani, akifunikwa na miiba ili kuikinga familia isiugue.

Kati ya miezi mitatu na mwaka mmoja baada ya mtu kufa, ilikuwa jukumu la ndugu wa karibu kusambaza mali zozote zilizoachwa na marehemu.

Hili lilifanyika katika sherehe ya kutoa urithi inayojulikana kama ‘ukubusya’ au ‘ukusenda ividwalo’ ambayo, kwa tafsiri sisisi ina maana “kuchukua nguo” za marehemu. Juhudi zaidi ilikuwa katika kumchagua mrithi, ambaye angekuwa kizazi cha wazee zaidi ya marehemu.

Hatimaye, kama mume amekufa, ‘urithi’ wa mjane ulijadiliwa na ndugu ambao wangekutana na kumtafuta mtu mwenye busara kulea familia. Mwanamke hakua na uchaguzi katika suala hili na ilikuwa lazima aolewe na yeyote aliyefikiriwa na familia yake.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au [email protected]

Chanzo: www.habarileo.co.tz