Baadhi ya Askari wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walioshiriki mapigano ya vita mbalimbali ndani na nje ya nchi wameiomba Serikali kuwaongezea kiwango cha pesheni ya kila mwezi ili kupunguza ukali wa maisha.
Ombi lingine walilolitoa wapiganaji hao leo wakati wa kumbukumbu ya mashujaa nchini yaliyoadhimishwa kwa ngazi ya Mkoa wa Pwani Mjini Kibaha ni kupewa nafasi ya kukaa na viongozi wa nyanja mbalimbali serikalini ili kuzungumza changamoto zinazowakabili hasa inapofikia wakati wa maadhimisho hayo.
“Tulipigana vita mbalimbali ikiwemo ya Iddi Amini na hata mataifa mengine lakini mchango wetu hivi sasa hautambuliki tunaishi kwa ugumu” amesema William Michael
Na kuongeza”Mfano ukiangalia pesheni tunayolipwa iko chini na haiongezeki tangu walivyotuongezea wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete”.
Kwa upande wake Abdulahamani Kiwanga amesema kuwa maaadhimisho ya siku ya mashujaa yanapaswa kuwahusisha wapiganaji wa vita kikamilifu kwani walifanya mambo makubwa ambayo ni matokeo ya hali ya amani inayaoendelea nchini mpaka sasa.
“Wenzetu wengi wameshatangulia mbele za haki ambao tulikuwa pamoja kwenye mapigano hivyo sisi tuliobaki ni vema tukathaminiwa kwa nyanja mbalimbali ikiwemo hata kuangalia maisha yetu ili tukabiliane na maisha”amesema.
Shehe wa Mkoa wa Pwani, Khamisi Mtupa amesema kuwa kitendo walichofanya mashujaa wakati huo ni ibada pekee kwani walikuwa wanapigania maisha ya wengi.
“Kuna baadhi yao wameshatangulia mbele za haki na wengine wanaishi katika hali ya ulemavu hiyo yote ni kwa ajili ya kupigania usalama wa maisha ya watu na jambo hilo ni ibada tosha na tunaamini hata nafsi za waliotutangulia ziko mahala pema” amesema
Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo MKuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema kuwa ili kuenzi mashujaa ni vema kila mwananchi akawa mstari wa mbele kuzuia vitendo vya uharifu vinavyovunja amani
Amesema kuwa ni vema wananchi wakatambua kuwa kazi ya kulinda usalama si ya askari pekee bali inapaswa kufanywa na kila mmoja kwa nafasi yake.