Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mwanza, Mrakibu wa Polisi Kamila Laban amesema miongoni mwa changamoto zinazopunguza ufanisi na kukwamisha shughuli za uokozi mkoani humo ni pamoja na kuwepo baadhi ya watu kupiga simu namba 114 na kuomba kuunganishwa Freemason na kutafutiwa wachumba.
Changamoto nyingine aliyoitaja ni uchelewaji wa taarifa majanga yanapotokea, na ujenzi holela wa makazi kukwamisha gari na maofisa wa jeshi hilo kufika eneo la tukio janga linapotokea.
Kamila amewataka watu wanaopiga simu hiyo kwa lengo la kufanya Mzaha kutofanya hivyo kwani kunasababisha upotevu wa muda ambao ungetumika kutoa huduma na kupunguza madhara kwa waaokutwa na majanga wakitafuta msaada
"Tupige simu namba 114 wakati wa Dharura, Wapo watanzania wenzetu anapiga simu halafu anauliza tu anataka kujiunga na Freemason mwingine anauliza mambo ya ajabu lakini wapo watanzania ambao wanapata shida za kweli kabisa za kuunguliwa na moto wakati wanapiga wanakuta simu iko busy kumbe ambaye amepiga ni yule anayetukana ni yule anayeomba wachumba , tunawaomba sana wananchi tuendelee kueleimika tuachane na hizi Tabia" - Amesema Kamila Laban