Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapare: asili, mila na mfumo wa maisha

A1757193be52c1663997a1be83b9840e Wapare: asili, mila na mfumo wa maisha

Fri, 22 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MAKALA ya leo yanaangazia jamii ya Wapare, kabila linalopatikana mkoani Kilimanjaro. Kabla ya kuingia huko, inasemekana waliishi maeneo ya Taita, Taveta na Ukamba nchini Kenya, na wakati huo walijulikana kwa jina la Waasu.

Masimulizi yanasema walipoingia Tanganyika, walitamani kufanya makao yao kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro, lakini wakavurumishwa na Wachaga waliokuwepo kabla yao. Wachaga hawakuwa radhi kuwaruhusu Wapare kuwa na makazi eneo hilo

Asili ya neno Wapare

Wakati wa kupambana walikuwa wakiambiana, “mpare… mpare!” wakimaanisha “mpige sana… mpige!” Waasu hawa wakatimka na kuelekea milima ambayo sasa inaitwa Milima ya Upare. Wakaanza kuitwa Wapare kwa maana ya “wapige”.

Hata hivyo, huo ni utani wa Wachaga kwa Wapare, na ni hadithi zinazosimuliwa na baadhi ya Wachaga ambao ndio watani pekee wa Wapare, utani uliozaliwa baada ya purukushani hizo za kuingia Tanganyika.

Lakini hakuna hata Mpare mmoja anayeafiki maelezo hayo, isipokuwa wanakiri kuwa walitokea Taveta: ndiyo maana hata baadhi ya maneno na lafudhi yao haiko mbali sana na maana halisi ya neno Wapare: watu wa Taveta.

Kutokana na tafiti za lugha na matamshi mbalimbali, matamshi ya neno la Kipare “mb” hubadilika na kuwa “p” katika Kiswahili. Kwa mfano Mbengo, kwa Kiswahili ni Pengo. Neno Mbinga, kwa kiswahili ni Pinga. n.k.

Hivyo neno Pare linatokana na neno “Mbare”, likiwa na maana ya ‘Kabila’, au Mkabila au hata mara nyingine katika kutofautisha aina za vitu. Hivyo Wapare walijiita “Vambare” wakiwa na maana ya “sisi wa kabila moja, tunaoongea lugha ya Chasu”. Hapo ndipo neno Vambare linabadilika katika Kiswahili na kuwa Wapare.

Katika lugha ya Kipare pia wanatambua makabila mengine kama Vashamba (Wasambaa); Vaagha (Wachaga); Vambughu (Wambugu); Vakwavi (Wamasai); Vakizungo (Wahaya); Vakamba (Wakamba); Vajaluo (Wajaluo) na wale ambao hawatambuliki kwa makabila yao huitwa Vanyika (au Mnyika kama ni mmoja).

Wapare wamegawanyika katika makundi mawili makubwa; Wapare wa Pare ya Kusini ambao ni Wapare wa Same, na Wapare wa Pare ya Kaskazini ambao ni Wapare wa Mwanga.

Hawa wa Pare ya Kaskazini nao wamegawanyika mara mbili: Wapare wa Ugweno (wanatumia lugha ya Kigweno) na Wapare wa Usangi (wanatumia lugha ambayo inatumiwa pia na Wapare wa Kusini ingawa inatofautiana kidogo katika matamshi).

Makao

Wapare wanatokea katika Wilaya za Same na Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro, lakini pia wapo katika wilaya ya Moshi sehemu za Kahe, Chekereni, Himo, Mabungo, Moshi Mjini, Wilaya ya Hai sehemu za Rundugai na Mto Weruweru. Pia wanaishi katika wilaya ya Lushoto, sehemu za Bumbuli na Mavumo.

Wapare ni miongoni mwa makabila ambayo watu wake wamesoma sana. Pia ni kabila la watu wanaopenda haki (yaani hawapendi kuonewa wala kumuonea mtu). Ndiyo maana watu wengine wanadhani wanapenda kesi, bali kesi ni njia mojawapo ya kuhakikisha haki inatendeka katika jamii.

Dhuluma kwa Wapare ni kitu kilichokuwa kimepigwa marufuku hata kwenye matambiko yao, japo siku hizi kuna uwezekano baadhi yao wakawa hawana sifa hii tena.

Dini

Zamani Wapare walikuwa na sala tofauti kwa kila ukoo na eneo lao la tambiko. Katika karne ya 19 hadi 20 wamisionari wa Ukristo waliingia maeneo mengi ya Upare.

Imani za Wapare kwa sasa zinatofautiana kutokana na maeneo: walio kusini mwa Wilaya ya Same katika maeneo ya Ndungu, Kihurio, Bendera, Hedaru, Makanya, Suji, Chome, Tae, Gonja, Mamba hadi Vunta wengi wao ni waumini wa Kanisa la Sabato.

Maeneo kama Chome, Mbaga, Gonja, Vudee yana waumini wengi wa Kanisa la Kilutheri. Katika Wilaya ya Mwanga kuna idadi kubwa ya Walutheri na Waislamu. Wakatoliki japo ni wachache, wanapatikana zaidi katika maeneo ya Kisangara Juu, Vumari, Gonja Kighare na Mbaga.

Shughuli za uchumi

Jamii za Wapare zimegawanyika katika makundi ya wafugaji na wakulima. Wakati wafugaji wengi walihamia katika tambarare za Upareni, wakulima wao waliishi milimani na wafuaji wa vyuma walikaa maeneo yote yaliyokuwa na uwezekano wa kupata chuma.

Walianza kufua chuma kabla ya mwaka 1700 na wafuaji waliitwa Washana, na huo ukoo upo hata leo hii. Wapare walikuwa wakiuza bidhaa zinazotengenezwa na chuma kama majembe, mapanga, visu, silaha kama mikuki kwa makabila ya jirani mfano Wachaga, na wamekuwa na uhusiano tangu siku nyingi. Bidhaa zao hizi ziliuzwa hata kwa Wasambaa.

Kwa asili Wapare hupeleka vijana wa kiume jando (mshitu) ambako walipata mafunzo jinsi ya kuishi na familia, japo siku hizi utamaduni huo hufuatwa na watu wachache.

Wapare ni wachapakazi sana wakichanganya kilimo, ufugaji na biashara, ndiyo maana hata leo wana uchumi mzuri katika viwango vya Tanzania.

Wapare pia wana ukaribu na makabila ya Mkoa wa Tanga hasa Wasambaa, Wazigua na Wanguu. Ukaribu wao uko katika lugha ambapo maneno mengi ya makabila haya yanafanana.

Vile vile hata majina ya baadhi ya maeneo yaliyopo kwa Wapare yapo pia kwenye maeneo wanamoishi Wasambaa na Wanguu. Kwa mfano, majina ya maeneo kama vile Gonja, Ndeme, Ndolwa n.k. yapo pia maeneo ya Wanguu na Wasambaa. Hii inaonesha kwamba makabila haya yana asili moja.

Mfumo wa maisha

Inasemekana Wapare ni kabila lenye ujasiri na ni watu wa kupanga kabla ya kutenda. Pia ni wavumilivu wenye kustahimili hali ngumu ya maisha ikiwa ni pamoja na njaa au kutokuwa na fedha.

Zamani za ukoloni waliweza kuungana na kufanya mgomo wa kukataa kodi zilizokithiri. Mgomo huo uliofanikiwa ulijulikana kama ‘mbiru’.

Kati ya mila na desturi zilizowajengea taratibu za kuwa na mifumo ya maisha ni zile walizoziita ‘Ndala’; ‘Msaragambo’; na ‘Kiwili’.

Ndala

Neno hili humaanisha utaratibu wa familia au watu wanaoishi jirani mno kula chakula kwa pamoja. Utaratibu wa Wapare ulikuwa kwamba kila mama anapotayarisha chakula kwa familia yake, ilibidi akitoe achanganye na chakula kingine cha wenzake na familia zote ziketi na kula pamoja.

Mfumo wa ndala kwa maana ya familia kula chakula kwa pamoja unaonekana kuwa na manufaa kwa kujenga uhusiano mwema baina ya familia na majirani katika kushirikiana; na pia kushirikiana katika kula kunachochea ushirikiano katika mambo mengine kama shida au raha.

Lakini pia watoto wanaokuzwa katika mfumo huo wanajengwa katika maadili mazuri wasiwe walafi na wachoyo maana wanazoea kuwa na wenzao na hii ndiyo sababu kabila hili lilikuwa na sifa ya kuwa wakarimu.

Watoto walifundishwa kuwa na nidhamu ya wakati wa chakula, kwa mfano kutonawa mikono au kuanza kula kabla ya wakubwa.

Msaragambo

Neno hili linamaanisha mfumo uliokubaliwa na jamii katika kitongoji, kijiji au kata wa kushirikiana katika kufanya kazi zenye faida kwa watu wote, maarufu kwa kazi za ujenzi wa taifa.

Kazi hizi ni za ridhaa na zilipaswa kwanza zikubaliwe na wengi vinginevyo haikuwa rahisi mtu mmoja kuitisha wito wa kazi fulani na watu wengine kuja kuifanya. Upo ushahidi wa kutosha kuhusu Wapare walivyotumia mfumo huu na kupata maendeleo makubwa wilayani mwao.

Zipo barabara za Mwanga hadi Ugweno na Usangi; Ndungu hadi Mamba na Vunta; Hedaru hadi Mwala; Makanya hadi Chome; Mpirani hadi Bombo Song’ana; Gonja Maore hadi Vuje na Vudee hadi Mbaga; Lembeni hadi Kilomeni.

Hata hivyo, si barabara tu, pia zahanati na shule nyingi zimejengwa na Wapare wa Wilaya za Same na Mwanga na kuinua kiwango cha maendeleo yao.

Kazi zilizofanywa kupitia utaratibu huu wa msaragambo ziliufanya Mkoa huu wa Kilimanjaro uongoze kwa maendeleo ya barabara nzuri, ujenzi wa shule nyingi hadi katika vitongoji.

Wapare si wapenda misaada ya mteremko ndiyo maana pamoja na kukabiliana na hali mbaya ya uhaba wa mvua mara kwa mara wamekuwa si watu wa kupiga yowe haraka.

Kiwili

Kiwili ni msamiati mwingine wa Kipare ambao ni mfumo wa maisha walioukubali katika kuendesha maisha ya familia na jamii zao kwa kusaidiana kazi.

Ni utaratibu ambapo familia au majirani hualikana ili kusaidiana katika kazi za kilimo, na hata mavuno hasa pale mmoja wao anapokuwa na kazi shambani mwake na kuhitaji msaada.

Siku hiyo, watu hukutana na kufanya kazi hiyo waliyoitiwa, mwenye kazi huandaa chakula ambacho watu watapata baada ya kumaliza kazi. Utaratibu huu ulikuwa na manufaa makubwa maana ulirahisisha kazi na kujenga moyo wa kusaidiana.

Kiwiri pia kiliweza kuitishwa na majirani kuwalenga wazee waliochoka au wagonjwa, ambao kwa namna moja au nyingine walionekana kushindwa kumudu kazi zao za shambani. Kupitia kazi za kusaidiana maisha ya familia nyingi za Wapare ziliokolewa na majanga ya kufikwa na njaa.

Mapacha kati ya Wapare

Kulikuwa na imani kuwa mwanamke akizaa watoto mapacha analeta mkosi na laana kwenye ukoo au mtoto akianza kuota meno ya juu.

Watoto hao waliuawa kwa kutupwa au kuegeshwa juu ya kilele cha jiwe kubwa pembezoni wakiwa wamelala baada ya kunyonyeshwa ama kulishwa uji na wazazi wao ambapo ni aghalabu mtoto kupona kwani akiamka na kujigeuza tu hudondoka toka juu hadi chini na kufa.

Maajabu ni kwa mtoto mmoja aliyeokotwa na Mzee Mgaya kule Ikamba na kumlea hadi akakua na kuwa Mtumishi wa Mungu jasiri na maarufu, marehemu Mchungaji Nathanieli Mgaya. Hadi leo hii mawe hayo yapo.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au [email protected]

Chanzo: habarileo.co.tz