Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapagazi 210 wapima Ukimwi mkoani Kilimanjaro

9900 Pic+ukimwi TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hai. Vijana zaidi 210 wanaojishughulisha na kuwabebea mizigo watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro (wapagazi) leo Jumapili Juni 24, 2018 wamejitokeza kupima Virusi vya Ukimwi (VVU).

Upimaji huo umefanyika katika lango la kupanda mlima huo na kuongozwa na madaktari wa hospitali ya Wilaya ya Hai.

Kaimu mganga mkuu wa hospitali hiyo, Irene Haule amesema mpaka kufikia saa 4 asubuhi, vijana 210 walikuwa wameshapima.

"Tunashukuru mwitikio umekuwa mzuri na wengi tuliowapima hawana maambukizi ya VVU na baadhi tuliowakuta na maambukizi tumewaunganisha  na vituo vya ushauri na kupewa dawa,” amesema.

Katibu wa Chama cha Wapagazi Tanzania (TPO),  Loshiye Mollel amesema tofauti na watu wanavyofikiri, wapagazi ni vijana wanaojitambua.

"Leo tupo hapa kufuatilia zoezi la utolewaji mikataba kwa makampuni yanayopandisha watalii lakini tumeona tushiriki pia kupima afya,” amesema.

Amesema chama hicho kina zaidi ya wanachama 19,000 ambao wote watapimwa afya zao kwa hiari.

“Tunaishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii na wizara inayosimamia kazi kuweka utaratibu wa kuhakikisha mpagazi kabla ya kupanda mlima anakuwa na mkataba,” amesema.

Mmoja wa wapagazi waliopima Ukimwi, Michael Kasunga amesema wamejitokeza kupima afya zao ili kuungana na kauli ya Serikali kutaka watu kupima afya zao.

“Tuliona Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) akizindua  zoezi la upimaji afya na baadaye wabunge na sisi tumeona tujitokeze,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz