Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waombwa kuimarisha kitengo cha mahakama inayotembea

30175d20037a5238c7046d751b409c37 Waombwa kuimarisha kitengo cha mahakama inayotembea

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imeishauri Mahakama Kuu Kanda ya Tanga iimarishe kitengo cha mahakama inayotembea ili kusaidia kumaliza migogoro ya ardhi na mirathi katika maeneo ya pembezoni.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga wa Tanga ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanasha Tumbo, aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama Kuu Tanzania.

Alisema kwenye Mkoa wa Tanga maeneo mengi ya pembezoni yanakabiliwa na changamoto ya migogoro ya ardhi hivyo upatikanaji wa huduma hiyo utarahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Tumbo alisema, mpaka sasa Mahakama hiyo imefika katika wilaya za Korogwe na Lushoto na bado kuna maeneo mengi yanayohitaji huduma hiyo.

"Huduma ya Mahakama inayotembea (mobile court) imesaidia kusogeza huduma karibu na wananchi pale ambapo hakuna huduma hivyo niwaombe huduma hii iweze kufika katika maeneo mengi ya pembezoni ambapo kuna changamoto" alisema.

Tumbo alisema, kitengo cha usuluhishi kimesaidia kumaliza mashauri ya madai kwa njia ya usuluhishi kabla ya kufika mahakamani na hivyo kuokoa muda na gharama ambazo zingetumika kuyasikiliza mahakamani.

Aliwataka wananchi na wadau kutumia kitengo hicho cha usuluhishi kusaidia kumaliza kesi kwa wakati sanjari na kuimarisha uhusiano baina ya mdai na mdaiwa na hivyo mashauri kumalizika kwa amani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga, Amiri Mruma, alisema maboresho yaliyofanywa na serikali ya kimiundombinu ikiwemo teknolojia yamesaidia kuimarisha utendaji kazi wa Mahakama.

Alisema maboresho hayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza muda wa mashauri mahakamani na hivyo wananchi kupata muda wa kuendelea na majukumu mengine.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Victoria Nogwa, alisema wameshaanza majaribio ya kuandika hukumu kwa lugha ya Kiswahili ili kutoa usaidizi kwa wananchi kufahamu kilichoamuliwa katika mashauri yao.

Chanzo: habarileo.co.tz