Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waomba serikali irejeshe mto kwenye skimu

13a991612d621cb79905d9fe98b25e81 Waomba serikali irejeshe mto kwenye skimu

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WANANCHI wa Kata ya Mng'aro iliyopo wilayani Lushoto mkoani Tanga wameiomba serikali kusaidia kutatua changamoto ya skimu ya maji ya kata hiyo iliyoharibika kutokana na kuhama kwa mto Umba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema eneo hilo ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya mahindi na Mpunga na kuharibika kwake kunawatia umaskini.

Diwani wa Kata ya Mng'aro, Jambia Shehoza alisema mafuriko yamehamisha uelekeo wa mto na hivyo wanaiomba Serikali iwasaidie kujenga upya miundombinu ya skimu ili wakulima waweze kuendelea na shughuli za uzalishaji.

"Tulikuwa tunalima kutokana na uwepo wa maji lakini sasa hatulimi kutokana na uhaba wa maji uliosababishwa na uharibifu wa miundombinu ya skimu" alisema Shehoza.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwebaya, Rodgers Kilango alisema kuwa kutokana na uharibifu wa skimu hiyo kwa sasa wananchi wa eneo hilo wanafanya kilimo cha kubahatisha .

Mkulima wa mpunga, Mwansiti Kinyashi alisema kuwa kwa sasa uzalishaji umekuwa hauna tija .

Hata hivyo Ofisa Ugani wa kata ya Mng'aro, Ramadhani Nyawenga alisema kuwa eneo hilo la kilimo kuna zaidi ya hekta 350 zilizokuwa zinalimwa mazao lakini kutokana na athari ya mvua eneo kubwa kwa wakati huu limeshindwa kulimwa.

Mbunge wa jimbo la Mlalo, Rashid Shangazi alisema kuwa tayari walishatoa taarifa katika Serikali ya mkoa wa Tanga na waliahidi kwenda kufanya tathimini katika eneo hili ili waone uharibifu uliokuwepo na hatua gani za kuchukua ili skimu hiyo iweze kutiririsha maji vizuri.

Jimbo la Mlalo ni moja ya majimbo matatu yaliyopo katika wilaya ya Lushoto ambayo huzalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara.

Chanzo: habarileo.co.tz