Watoto 11 wilayani Handeni mkoani Tanga wamenusurika kufa baada ya kula matunda yanayodaiwa kuwa na sumu.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Mganga wa zamu wodi ya watoto Hospitali ya Mji Handeni Steven Julius amesema ni kweli wamepokea watoto 11 jana Februari 11,2023 wakiwa wanaumwa na baada ya uchunguzi walibaini kuwa watoto hao wamekula matunda yenye sumu.
Steven amesema kuwa mpaka leo asubuhi watoto wote 11 walikuwa wanaendelea vizuri na kuruhusiwa mchana kurudi nyumbani baada ya kuonekana maendeleo yao ni mazuri.
"Tulipokea watoto 11 inasemekana walikula matunda ambayo hayaliwi, hakuna mtoto aliyepata madhara makubwa sana walikuwa na hali ya kulegea na kutapika ila baada ya uchunguzi ilibanikia ni mchafuko wa tumbo kwa kula matunda hayo na wanaendelea vizuri." amesema Dokta Steven.
Mmoja wa wazazi wa watoto hao, Lydia Msigwa amesema miti hiyo ipo muda mrefu ila wameshangaa jana jioni, kuona watoto wanatapika na baada ya kuwauliza wakasema wamekula matunda yaliopo nyumbani hapo.
"Hii miti ipo hapa muda mrefu na haijawahi kuleta madhara ila tumeshangaa jana watoto wamepata tatizo la kula haya matunda maana kila mtoto ukimuangalia anatapika na kulegea, ndio tumegundua yana madhara." amesema Lydia
Amesema watoto wakiulizwa kuhusu matunda pori hayo wanasema ni korosho mpya wanapasua na kuchukua tunda la kati kati ambalo wanahisi ndio lenye madhara.
Mtendaji kata ya Vibaoni, Zainabu Mhanga amesema kutokana na athari hiyo wameanza zoezi la kukata miti hiyo kwenye jamii, lengo ni kuhakikisha lisitokee tena kwani watu wamepanda kama uzio.
Tukio hilo ni la pili kwa kata ya Vibaoni watoto kula matunda hayo na kudhurika na la tatu ambapo kata ya Kwenjugo iliwahi kutokea pia na watoto kukimbizwa hospitali.