Mtu mmoja amelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito wilayani Mikumi na wengine wametibiwa na kuruhusiwa baada ya basi la kampuni ya Golden Deer walilokuwa wakisafiria kutoka Kyela kwenda Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka.
Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema kuwa ajali hiyo imetokea leo Jumatatu Agosti 7, 2023 jioni eneo la Msimba kwenye mteremko na kona za Iyovi Mikumi ambapo amemtaja majeruhi kuwa ni Elinipenda Kishimbo (26) aliyeteguka mkono.
Kamanda Mkama amemtaja dereva wa basi hilo kuwa ni George Obedi (48) huku chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni uzembe wa dereva huyo kwa kuwa alitaka kulipita gari lililokuwa mbele yake bila ya kuchukua tahadhari na hivyo kukutaka na gari jingine uso kwa uso.
"Huyu dereva bila kujali kuwa eneo lile ni hatari alilipita gari lililopo mbele na kabla hajalipita likatokea gari jingine mbele alichoamua ni kwenda kulia zaidi mwa barabara na hivyo alishindwa kulimudu basi hilo hasa ukizingatia alikuwa kwenye mteremko mkali," amesema Kamanda Mkama.
Hata hivyo amesema kuwa tayari dereva huyo anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi huku na uchunguzi utakapokamilika taratibu za kumfikisha mahakamani zitafuata.