Kigoma. Watu wanne wamefariki dunia na wengine 42 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wamepanda kuacha barabara na kupinduka mkoani Kigoma.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno amesema ajali hiyo imetokea jana Jumatano Januari 23, 2019 majira ya saa nne usiku ambapo basi la Fikosh lenye namba ya usajili T 400 AUV lilipinduka katika eneo la Mnarani katika kijiji cha Uvinza, wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Basi hilo lilikuwa linatoka Mwanza kwenda mkoani Kigoma kupitia mikoa ya Shinyanga na Tabora.
Ottieno amesema kati ya waliokufa wanaume ni watatu na mwanamke mmoja ambao hadi sasa hawajatambuliwa na maiti zimehifadhiwa katika kituo cha afya Uvinza.
Majeruhi wote 42 wapo katika hospitali ya mkoa wa Kigoma, Maweni ambapo 12 hali zao ni mbaya na wengine 30 wanaendelea vizuri baada ya kupata majeraha ya kawaida.
"Chanzo cha ajali ni mwendokasi uliosababisha dereva wa basi hilo, Abdallah Ramadhani kushindwa kulimudu kwenye kona na matokeo yake likaacha barabara na kupinduka," amesema Ottieno.